Chama cha ANC Afrika Kusini chamtimua Malema

Julius Malema

CHAMA tawala cha ANC nchini Afrika Kusini kimemtimua rasmi kiongozi wa Jumuiya ya vijana katika chama hicho, Julius Malema, baada ya rufaa ya kupinga uamuzi wa kutimuliwa kwake hapo awali kutupiliwa mbali.

Kamati ya Nidhamu ya ANC ilitoa uamuzi huo baada ya kusikiliza rufaa iliyowasilishwa na Malema dhidi ya kutimuliwa kwake uanachama kwa kipindi cha miaka mitano kwa makosa ya kuleta mgawanyiko.

Kamati hiyo ikiongozwa na kiongozi mkongwe na mfanyibishara, Cyril Ramaphosa, iliangalia tena rufaa aliyokata, Malema na bado ikabaini makosa ya kukigawanya chama cha ANC ikiwa ni pamoja na kukitia aibu chama.

Hata hivyo, Malema katika siku za awali ameelezea wazi kwamba atakata rufaa iwapo kamati hiyo itamsimamisha kujihusisha na shughuli za chama cha ANC. Pamoja na hayo Malema bado anaweza kukata rufaa katika kipindi cha miaka 14.

Julius Malema amekuwa akisisitiza kuwa anaonewa kwa sababu anataka chama hicho kutaifisha migodi ya nchi hiyo. Pia anasema baadhi ya watu katika chama cha ANC hawamtaki kwa sababu anataka chama hicho kupata kiongozi mpya katika mkutano wake baadaye mwaka huu ili kuchukua nafasi ya Rais Jacob Zuma kuondoka.
-BBC