Na Mwandishi wa dev.kisakuzi.com, Arumeru
MTOTO wa aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, marehemu Jeremiah Sumari (CCM), Sioi Sumari leo ameibuka tena mshindi katika kura za maoni zilizopigwa kati ya wagombea wawili waliozua utata hivi karibuni.
Sioi Sumari ameibuka mshindi kwenye uchaguzi huo baada ya kujipatia kura 761 kati ya kura 1122 zilizopigwa na wajumbe wote walioshiriki katika uchaguzi huo wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi kumpata mgombea atakaye peperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, utakaofanyika Aprili Mosi, mwaka huu.
Mgombea mwenzake, Wiliama Sarakikya waliyokuwa wakipambana vikali na Sioi ameambulia kura 361. Awali akitangaza matokeo hayo leo mjini Arumeru, eneo la Usa River, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, alisema kuwa Sioi amejipatia kura 761 huku mgombea wa pili, Sarakikya akijinyakulia kura 361 kati ya jumla ya kura 1124 zilizopigwa na wajumbe.
Msekwa alisema idadi ya wapiga kura ilikuwa 1124 na kura mbili ziliharibika hivyo kura halali kusalia 1122. Hata hivyo kabla ya kumtangaza mshindi huyo, Msekwa aliwaeleza wajumbe kuwa ameridhika na taratibu wa uchaguzi huo.
Muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi (Sioi) wajumbe wengi walisikika wakishangilia, huku wengine wakimbeba kutoka ukumbini kitendo kilichoonesha alikuwa na wajumbe wengi wanaomuunga mkono.