Benki, asasi za fedha ondoeni masharti magumu-Wajasiriamali

Na Mwandishi Wetu
Moshi

BENKI na asasi mbalimbali zinazojihusisha na kutoa mikopo zimetakiwa kulegeza masharti ya mikopo hiyo ili kuwawezesha wajasiriamali wengi kupata huduma hiyo kirahisi na hivyo kuongeza mitaji yao, tofauti na ilivyo sasa.

Wito huo umetolewa juzi mjini hapa na Waziri wa viwanda, Biashara na Masoko ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Dk. Cyril Chami wakati wa ufunguzi wa maonesho ya bidhaa za viwandani yaliyohusisha wajasiriamali wadogo na kufanyika Wilayani Moshi.

Chami alisema kuwa hata nchi zilizoendelea zilianza katika hatua ya chini kama wajasiriamali na kupanda hadi kufikia walipo sasa, hivyo kuwataka waendelee kuonesha uthubutu katika kujiendeleza kwenye vikundi mbalimbali.

Waziri huyo aliwataka wajasiriamali kuondokana na dhana potofu kuwa Mtanzania hawezi kumiliki kiwanda kwa kudhani viwanda ni lazima vitokane na wawekezaji pekee jambo ambalo alidai si kweli bali linawezekana tena kirahisi kutokana na kukua kwa teknolojia nchini.

“Tanzania sasa tumefikia mbali kiteknolojia, mashine na bidhaa zilizopo hapa ni maendeleo tosha, natamani ifikie mahali bidhaa zetu ziuzwe kwa kiwango kikubwa nchi za nje hivyo kukuza uchumi wa nchi na wajasiriamali wenyewe,” alisema Dk. Chami.

Kwa upande wao wajasiriamali hao mbali na kulalamikia masharti magumu kutoka kwenye benki na asasi za mikopo, pia walimweleza waziri huyo kuwa wanakabiliwa na uhaba wa maeneo ya kufanyia kazi, mitaji ya kutosha kununua mashine za kisasa ili kukabiliana na teknolojia pamoja na masharti magumu ya kupata leseni hasa kwa wasindikaji wa vyakula.

Mmoja wa wajasiriamali hao, Seth Moshi alisema kuwa upatikanaji wa malighafi umekuwa mgumu hivyo wakati mwingine kushindwa kukidhi mahitaji ya wanunuzi wao na kuitaka Serikali kuwasogezea huduma hiyo karibu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inapatikana kwa bei ambayo wataimudu.

Maonesho hayo yaliyodhaminiwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) yanafanyika kwa siku sita huku lengo likiwa ni kutangaza bidhaa zao kwa wakazi wa Mjini wa Moshi na maeneo ya jirani.