Na Magreth Kinabo – MAELEZO
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa magari saba ya huduma za mkoba kwa ajili ya wananchi wengi kupata huduma za madaktari bingwa hususan walioko vijijini.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda wakati akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kukabidhi magari hayo kwa wawakilishi wa hospitali mbalimbali kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo.
“Tunagawa magari haya kwa madhumuni ya kupeleka huduma za wataalamu bingwa karibu na wananchi. Lengo la Serikali ya Awamu ya Nne ni kuhakikisha huduma za afya na ustawi wa jamii zinawafikia nchinii kote na hasa vijijini, ambako ndipo wanapoishi wananchi wengi. Haya magari yatatumiwa na madaktari bingwa katika kanda zetu zote nchini kote,” alisema Waziri Mponda.
Aliitaja thamani ya magari hayo kuwa ni sh. milioni 181 kwa kila mmoja ambayo inahusisha pamoja na vifaa vilivyoko ndani ya gari.
Waziri Mponda aliongeza kuwa watumishi kutoka hospitali husika watafundishwa namna ya kutumia magari hayo ambayo yana vifaa maalaum vipya vya kisasa, ambao watawaelekeza wenzao wakati wa kliniki hiyo.
Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni vya kufanyia uchunguzi na vya kutolea huduma. Magari hayo pia yana jenereta kwa ajili ya kupata umeme sehemu ambazo hazitakuwa na umeme. Hospitali zilizopata magari hayo za Kanda ya Mashariki ni CCBRT Dar es Salaam, Kasikazini KCMC Kilimanjaro, Kati Chuo Kikuu cha Dodoma Kusini Rufaa ya Mbeya, Kusini Mashariki Ndanda Mtwara, Magharibi Maweni Kigoma na Ziwa Bugando.
Wakizungumzia kuhusu magari hayo wawakilishi wa hospitali hizo walisema wanaishukuru serikali kwa kuwa utawezesha wananchi wasioweza kufikia huduma za afya kuzipata kwa kiurahisi.