‘Siasa zisiingizwe kwenye shughuli za maendeleo’

Na Anna Nkinda, Maelezo
Mkuranga

WANANCHI wilayani Mkuranga wametakiwa kuachana na itikadi za kisiasa katika shughuli za maendeleo, kwani suala la maendeleo linamgusa kila mwananchi bila kujali itikadi za kisiasa.

Wito huo umetolewa jana mjini hapa na mke wa Rais, Salma Kikwete wakati akifungua Chama Cha kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) kitakachojulikana kama ‘Salma Kikwete’ kilichopo kijiji cha Hoyoyo Mkoa wa Pwani.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema hivi sasa wananchi wanatakiwa kuachana na masuala ya kampeni za uchaguzi na kujishughulisha zaidi na mambo ya maendeleo bila kubaguana kwani kipindi hicho kimepita tangu mwaka 2010.

“Nataka mfahamu kuwa SACCOS ni chombo cha kujiletea maendeleo hata kama chimbuko lake ni ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wewe kama utakataa kujiunga na SACCOS hii kwa madai kuwa mbona ina jina la mama Kikwete, mbona imefunguliwa na mke wa rais shauri yako wenzako watajiunga, watapata fedha na kuzifanyia shughuli za maendeleo huku wewe ukibaki kama ulivyo,” alisema Mama Kikwete.

Aidha Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwaasa wanachama wa SACCOS hiyo kuitumia vizuri mikopo watakayoipata katika shughuli za maendeleo kama kuongeza mitaji ya biashara, kuboresha shughuli za kilimo na makazi pamoja na kuboresha maisha ya familia zao kwani kufanya hivyo ndiyo manufaa ya SACCOS.

“Mkitumia vibaya mikopo mtakayoipata mtashidwa kuboresha maisha yenu na wakati mwingine kushindwa kurudisha fedha mlizokopa, ambazo wanachama wengine wanazihitaji na mnaweza kuiua kabisa SACCOS yenu,” alisema.

Aliwaomba wataalamu wa biashara wawe karibu na wananchi ili kuwapa elimu ya sahihi ya kuendesha biashara na hatimaye biashara zao ziweze kuwapatia faida nzuri na kuweza kurejesha fedha walizokopa.

Wanachama wengi wa SACCOS hiyo wanategemea shughuli za kilimo, lakini Mama Kikwete amewashauri pia kuendesha biashara ndogondogo, ambazo zitawasaidia kupata mahitaji muhimu ya familia ili kuongeza kipato zaidi.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mkuranga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini, Adam Malima alisema jambo la msingi wanaloliangalia ni amna ya kumkomboa mwananchi kutoka katika hali ya maisha duni na kuishi maisha yatakayompatia kipato cha kila siku na hivyo kujikwamua na umasikini.

“Ninakupongeza sana (Mama Kikwete) kwa jitihada zako unazozifanya za kuwakomboa wananchi hasa waishio vijijini nasi tunakuunga mkono kwa kuwahimiza wananchi waone umuhimu wa kujiunga na vikundi mbalimbali vya maendeleo kwani kwa kufanya hivyo watakopa na kupata fedha ambazo zitawasaidia katika maendeleo,” alisema Malima.

Akielezea historia ya SACCOS hiyo Mweka Hazina, Somoye Kilimile alisema imetokana na wazo la Mama Kikwete la kutumia sehemu ya shamba lake kama kituo cha mafunzo ya kilimo na ufugaji alichokizindua Februari 23, 2008 kama shamba darasa kwa ajili ya kujifunza uzalishaji wa zao la pilipili baridi (paprika), migomba, miembe ya kisasa na ufugaji wa kuku wa kienyeji chini ya usimamizi wa taasisi ya WAMA na pia viongozi wa Hoyoyo na Wizara ya Kilimo.
SACCOS hiyo ina wanachama 103 kati yao 65 ni wanawake na 38 ni wanaume.