Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete Februari 29, 2012, ametangaza kuwa ametoa mwaliko kwa wadau mbalimbali kuwasilisha majina ya watu ambao wadau hao wanawapendekeza kuwamo katika Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni kuhusu Katiba Mpya.
Wadau waliopatiwa mwaliko huo, kwa kutumia Gazeti la Serikali Namba 66 la Ijumaa ya Februari 24, 2012, ni pamoja na vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Jumuia za Kidini, Asasi za Kiraia pamoja na Jumuia, Taasisi na makundi mengine yenye malengo yanayofanana.
Rais ametangaza kutoa mwaliko huo katika Hotuba yake ya mwisho wa Mwezi Februari, 2012, ambayo ameitoa jioni ya leo Ikulu, Dar es Salaam.
Rais ametoa mwaliko huo kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyopitishwa Februari 10, mwaka huu na kikao kilichopita cha Bunge, na kutiwa saini na yeye mwenyewe Februari 20, mwaka huu, 2012.
Kwa mujibu wa mwaliko huo ambao pia utatangazwa katika magazeti ya kawaida, wadau hao wanatakiwa kupendekeza majina ya watu wasiozidi watatu wanaokidhi sifa zilizotamkwa katika kifungu cha sita cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Sifa hizo ni kama zifuatazo:
(a) Uzoefu katika kufanya mapitio ya Katiba na sifa za kitaaluma za wajumbe kwenye mambo ya Katiba, Sheria, Utawala, Uchumi, Fedha na Sayansi ya Jamii. (b) Jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na (c) Umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbali mbali ya kijamii.
Rais pia ameelekeza kuwa majina ya wanaopendekeza yawasilishwe kwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Muungano ama kwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mwisho wa kupokea majina hayo ni Machi 16, 2012.
Baada ya hapo, Mheshimiwa Rais atashauriana na Rais wa Zanzibar juu ya uteuzi wa wajumbe pamoja na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Tume itakuwa na wajumbe 30 (mbali ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti) na watapatikana kwa idadi sawa ya wajumbe 15 kutoka kila upande wa Jamhuri ya Muungano.