Chadema wamchagua Nassari Arumeru

Mgombea wa CHADEMA, Joshua Nassari

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemchagua Joshua Nassari kupeperusha yake katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, utakaofanyika Aprili Mosi, mwaka huu.

Akitangaza matokeo ya uteuzi huo, Mkurugenzi wa Bunge na Oganaizesheni wa Chadema, John Mrema alisema Nassari ameteuliwa baada ya kupata kura 805 sawa na asilimia 90.6 ya kura zote 888 zilizopigwa.

Alisema Nassari aliwaangusha Anna Mghiwa aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata kura 23, akifuatiwa na Godluv Simba (18), Rebecca Magwisha (12), Samweli Shami (10), Anthony Mussari (8) na Yohanne Kimuto (6).
“Kura zilizopigwa zilikuwa 888 zilizoharibika ni sita na wagombea wote wametangaza kukubali matokeo,” alisema Mrema. Msimamizi wa uchaguzi huo alikuwa ni mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei.
Ukumbini

Mgombea Musari aliyehamia Chadema baada ya kuangushwa kwenye mchakato wa kutafuta mgombea kupitia CCM aliwaambia wajumbe kwamba, tayari alikwishafukuzwa kazi ya ukuu wa shule hivyo aliomba wajumbe wampigie kura kupeperusha bendera ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini katika uchaguzi huo.

Kauli ya mgombea huyo ilimfanya mmoja wa wajumbe kutoka kata ya Maji ya Chai kumhoji iwapo hatahama tena Chadema akikosa kura katika uchaguzi huo wa jana, naye akaahidi kushirikiana na wana Chadema wenzake kutafuta ushindi wa chama chake hicho.

Awali, mzee Mtei alisema chama hicho kinahitaji wabunge wenye kuendesha na kutekeleza sera zinazojibu mahitaji ya wananchi na jamii wanayoongoza kwa kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wote bila kujali tofauti miongoni mwao.

“Hivi sasa wananchi wengi wanakula mlo mmoja kwa siku sababu hawawezi kumudu gharama ya milo miwili na hili linasababishwa na usimamizi na uongozi mbovu wa Serikali ya CCM,” alisema Mtei.

Aliwaasa wana Arumeru kupuuza rushwa inayodaiwa kuwa imeanza kusambazwa sehemu mbalimbali za jimbo hilo na wanaodaiwa kuwa viongozi au wanachama wa CCM na kuchagua kiongozi wanayeamini kuwa atawakilisha hoja na fikra zao bungeni bila kushaiwishiwa kwa rushwa.

CCM wakamatwa kwa rushwa
Katika hatua nyingine, viongozi watatu wa CCM, wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa kuhusiana na kura za maoni za marudio ndani ya chama hicho.
CHANZO: Mwananchi, kusoma zaidi tembelea www.mwananchi.co.tz