Ushirikiano na UN unamchango mkubwa kimaendeleo-Dk Shein

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema ushirika uliopo kati ya Umoja wa Mataifa na Tanzania umekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza sekta za maendeleo mjini Zanzibar.

Dk. Shein aliyasema hayo jana alipokuwa na mazungumzo na Wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa waliopo Tanzania wakiongozwa na Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Alexio Musinde. Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein aliwaeleza Wawakilishi hao kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na mashirikiano kutoka kwa Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa ambayo yameweza kuiunga mkono Zanzibar kwa muda mrefu.

Alisema kuwa Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yameweza kuchangia kwa kiasi kikubwa sekta za maendeleo hapa nchini na kuwa chachu ya maendeleo endelevu.
Dk. Shein aliwaeleza Washirika hao wa Maendeleo kuwa miradi kadhaa imeweza kuimarika sanjari na kwajengea uwezo wafanyakazi wa sekta mbali mbali za maendeleo na kuweza kupata mafunzo ndani na nje ya Zanzibar.

Akitoa maelezo kwa upande wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia nyumba na Makaazi, Dk. Shein alisema kuwa mikakati madhubuti imewekwa katika kuhakikisha masuala ya ujenzi holela na watu kuchukua sheria mikononi mwao yanafanyiwa kazi ili kuuweka mjini katika mazingira mazuri.

Alisema kuwa kuwepo kwa mashirikiano mazuri kati ya Serikali na Shirika hilo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuweka mipango mizuri ya miji na makaazi ya watu hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ni mji wenye kivutio kikubwa cha utalii.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar imekuwa na mashirikiano mazuri na Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), na kutoa pongezi kwa juhudi za shirika hilo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya afya.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa Mashirika ya UNWOMEN, IOM, UNIDO, UNESCO, ILO, FAO, UNAIDS ambayo wawakilishi wake ndio waliofanya mazungumzo nae hivi leo na Mashirika mengineyo yameonesha juhudi zao katika kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha miradi ya maendeleo na kutoa shukurani kwa mashirika hayo.

Nao Wawakilishi wa Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa walimueleza Dk. Shein mikakati yao waliyoiweka katika kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kueleza kufarajika kwao na mashirikiano wanayoyapata kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Katika mazungumzo hayo kila Mwakilishi alimueleza Dk. Shein jinsi Shirika lake lilivyojipanga katika kuisaidia Zanzibar na kuthamini juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein.

Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Mwakilishi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), anayefanya kazi zake hapa Tanzania Bi Diana Ellen Tempelman. Katika mazungumzo hayo, Mwakilishi huyo wa FAO, alimueleza Dk. Shein kuwa amefurahishwa na mipango, taratibu, sera na hatua za uhifadhi wa chakula Zanzibar na kusisitiza azma ya Shirika hilo ya kuzalisha chakula zaidi sanjari ya kukiimarisha kilimo cha umwagiliaji maji.

Naye Dk. Shein alimueleza Mwakilishi huyo juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kukiimarisha chuo cha Kilimo Kizimbani ili kiweze kutoa wahitimu bora na wenye sifa kwa lengo la kuendeleza kilimo nchini.

Aidha, alimueleza hatua zinazochukuliwa katika tafiti mbali mbali ikiwemo za mbegu na kumueleza jinsi hatua zinavyochukuliwa katika kuiimarisha mbegu mpya ya mpunga ya NERICA, uhifadhi wa chakula, mbegu bora, pamoja na kupunguza bei za pembejeo wakulima na kuweka miundombinu bora ya kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji.

Sambamba na hayo, alimueleza juhudi za kuongeza uzalishaji wa chakula, kupitia Sheria ya Uhakika wa Chakula na Lishe ya mwaka 2011, kwa kuanzisha maghala ya akiba ya chakula, ili iweze kuchangia katika kupunguza mumko wa bei, kwa kuongeza chakula kinachoingia katika soko wakati wa upungufu wa chakula.