Sezibera asema ndoto ya EAC kuwa na sarafu moja kutimia

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Na James Gashumba wa EANA, Arusha

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk. Richard Sezibera amesema nchi wanachama wa jumuiya hiyo wamejizatiti kuhakikisha kwamba ndoto ya kuwa na sarafu moja inakuwa ya kweli.

Alisema licha ya majadiliano yanayoendelea hivi sasa juu ya Itifaki ya Sarafu Moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAMU), nchi wanachama wameongeza kasi ya kujiandaa katika kuoanisha masuala ya fedha na sera za ubadilishanaji fedha, mfumo wa malipo na kuweka mfumo wa sekta ya fedha wa kikanda ili kuunda soko moja la fedha.

“Napenda kusema wazi kwamba tulichojifunza kutokana na mgogoro wa fedha wa Ulaya kama ilivyokuwa kwa jumuiya nyingine za kiuchumi za kikanda, umekuwa ni funzo la kuimarisha na kujenga Umoja wa Fedha wa EAC,” alisema.

Katibu Mkuu huyo alikuwa anafungua mkutano wa kanda baina ya EAC na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuhusu kuoanisha sekta ya fedha ulioanza Jumatatu, Februari 27, 2012.

Mkutano huu uliojumuisha wajumbe na wataalamu mbalimbali wa sekta ya fedha una lengo la kujadiliana juu ya hali ya sasa, mafanikio na matarajio ya EAC juu ya kuoanisha sekta ya fedha katika kanda hiyo. Dk. Sezibera aliipongeza IFM kwa msaada wake wa kiufundi na misaada mingine katika mchakato mzima wa kuanzisha sarafu moja.

“Ni heshima ya pekee kwa EAC kupewa nafasi ya kuwa mwangalizi katika vikao vya IFM, hatua ambayo ni ishara kwamba Shirika linatuamini. Napenda kulihakikishia Shirika hili kwamba nchi wanachama wa EAC, zimejizatiti kuhakikisha kwamba ndoto ya EAC ya kuwa na sarafu moja inakuwa ya kweli,” aliongeza.

Alielezea matumaini yake kwamba mkutano huo utajadili pia namna ya kuepuka makosa yaliyofanyika katika mgogoro wa fedha wa Ukanda wa Ulaya. Wajumbe wa mkutano huo ni pamoja na wadau wa mtangamano wa EAC na wabia wa maendeleo duniani, wakiwemo watunga sera, wasomi na watafiti, viongozi wa masuala ya biashara na mashirika ya kiraia.