Dk. Shein asema mradi wa Elimu wa Karne ya 21 ni chachu ya maendeleo Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

UZINDUZI wa Mradi wa Elimu wa Karne ya 21, unaohusisha Elimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa shule za msingi Zanzibar ni chachu ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kijamii katika ulimwengu huu wa utandawazi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo jana katika uzinduzi wa Mradi wa Elimu ya Lazima wa Karne ya 21, hafla iliyofanyika huko katika Skuli ya Mwanakwerekwe C, mjini Zanzibar.

Katika uzinduzi huo ambao viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Shairif Hamad, Balaozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Alphonso Leinhardt, Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar ikiwa ni sehemu ya dunia haiwezi kujiengua katika hilo.

Dk. Shein alisema kuwa Mradi wa kufundishia na kujifunzia kwa skuli za msingi kwa kutumia kompyuta kuanzia darasa la kwanza hadi la nne utawaandaa watoto katika kukabiliana na ulimwengu wa kileo.

Alisema kuwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ina umuhimu mkubwa kwa ulimwengu wa sasa na hasa kwa watoto katika kukuza elimu yao ambapo hatua hiyo itawasaidia katika ugunduzi wa maarifa mapya katika masomo, kuchemsha bongo, kurahisisha ufanyaji wa kazi zao na kuokoa muda.

Dk. Shein apia alisisitiza kuwa mabadiliko haya ya kielimu yanategemea sana mchango wa walimu, wenye kubadilika kitaaluma na katika mbinu za ufundishaji na kueleza kuwa lazima walimu wajifunze kutumia vifaa vya kisasa yakiwemo matumizi ya Kompyuta.

“Huu si wakati wa mwalimu kufundisha kwa mbinu ya “Chalk and talk”, Nawasihi walimu wote waitumie fursa ya Mradi huu na wao kujiendeleza”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali itaendelea kuwatengenezea mazingira bora walimu ili wazidi kupata moyo katika kutekeleza majukumu yao na kutoa wito kwa walimu kuendelea kuchapa kazi, na wawe tayari kubadilika na kujitahidi kuzingatia maadili mema na kwua watu wa kuingwa na waadilifu na kuwa mfano bora kwa watoto wanaowafundisha.

Dk. Shein alieleza kuwa kwa kutambua umuhimu wa hilo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imedhamiria kwa dhati kuongeza matumizi ya teknolojia ya ya Habari na Mawasiliano katika elimu na nyanja nyengine za kiutumishi.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itazidi kujitahidi katika kuongeza nafasi zaidi, vifaa vya kisasa na walimu ili lengo la kuimarisha elimi ncghini liweze kufikiwa na kusisitiza kuwa kila mtoto aliyefika umri wa kuanza skuli atapatiwa fursa hiyo bila ubaguzi wa aina yoyote.

Dk. Shein alipongeza uwamuzi wa Serikali ya Marekani kwa kupitia Shirika lake la Maendeleo (USAID) kwa kutoa msaada huo muhimu unaogharimu Dola za Kimarekani milioni 50 ambao utakuwa wa miaka mitano pia, aliupongeza uongozi wa Wizara ya Elimu uliopo na uliopita kwa kushirikiana na washirika hao wa Maendeleo.

Pia,alitoa pongezi kwa Kampuni kubwa za Kimataifa ambazo nazo zimechangia juhudi za Serikali ya Marekani katika kuunga mkono Mradi huo kwa kutoa huduma zao ikiwemo Kampuni ya Microsoft, CISCO, Intel na Kampuni ya ZANTEL pamoja na kulipongeza Shirika la “Creative Associates” la Marekani kwa kusimamia Mradi huo.

Nae Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe.Alfonso Lenhardt alisema kuwa Mradi huu ni msingi muhimu wa kuleta mabadiliko makubwa ya teknolojia ya habari na mawasilaino hapa Zanzibar.

Aidha, Balozi Lenhardt alisema kuwa elimu ina umuhimu sana kwa vijana wa Tanzania kwani ndio silaha katika maisha yao na kusisitiza kuwa mradi huo utakapomalizika unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya walimu 4,094, skuli za msingi na sekta za elimu.

Nae Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Zahra Ali Hamad alisema kuwa Mradi huo utaweza kuwasaidia walimu na wanafunzi kupata taaluma ya teknolojia ya habari na kuzidisha uimarishaji wa sekta ya elimu nchini.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Bi Mwanaidi Saleh alieleza kuwa mbali ya kushughulikia utoaji wa elimu kwa walimu na wanafunzi, mradi huo pia unahusika na kuweka utaratibu mzuri wa kukusanya taarifa na takwimu ya masuala ya elimu.

Alisema kuwa Mradi wa matumizi ya teknolojia ya kisasa katika elimu utahusisha skuli 248 za msingi, kati ya hizo skuli 45 zitapatiwa vifaa zaidi kwa mujibu wa sifa zilizowekwa ambapo majaribio ya Mradi yameanza katika skuli ya Kisiwandui na Daraji na Kituo cha Walimu Michakaeni.

Alisema kuwa skuli zote zitapatiwa Kompyuta na kuunganishwa na mtandao ambapo taarifa na takwimu za skuli na za elimu zitapatikana ambapo pia vituo vyote 10 vya walimu vitapatiwa vifaa vya kisasa ili viweze kutoa mafunzo kwa walimu kwa ufanisi zaidi.

Mapema Dk. Shein alitembelea chumba cha maonesho na kupata maelezo juu ya Mradi huo ambao Mkoa Mtwara nao unanufaika kwa Tanzania pamoja na kuwangalia watoto na kupata maelezo kutoka kwa walimu husika jinsi mafunzo yanavyoendeshwa kwa watoto hao wadogo kupitia taaluma za mradi huo.