Na Mwandishi Wetu, Moshi
IMEBAINIKA kuwa baadhi ya wananchi waishio maeneo ya mipakani mwa nchi, wamekuwa na tabia ya kuharibu mipaka hiyo kwa kuondoa mawe yaliyowekwa mipakani.
Kutokana na tabia hiyo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo na
Makazi, Goodluck Ole Medeye, ameagiza wananchi wote waishio na maeneo ya mipaka ya kimataifa kuacha mara moja shughuli zozote ndani ya mipaka ambazo zinaharibu mazingira.
“Wananchi wa maeneo ya mipaka ya kimataifa wanatakiwa kuacha mara
moja, shughuli za kilimo, uchimbaji na kujenga kwani kwa kufanya hivyo
ni kinyume na sheria, na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya
wale watakaobainika,” alisisitiza kiongozi huyo.
Aidha wananchi hao wamebainika kuwa wamekuwa wakijishughulisha na
shughuliza uchimbaji wa miamba katika maeneo hayo na kutengeneza
matofali jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likichangia uharibifu
wa mazingira.
Naibu Waziri alibaini hayo wakati alipokuwa akikagua mpaka baina ya
Tanzania na Kenya, katika eneo la Rombo mkoani Kilimanjaro, juzi.
Aidha katika mpaka huo Naibu huyo alishangazwa na tabia yaa baadhi ya watu ambao wameng’oa mawe makubwa yaliyowekwa mipakani wakidhani kuwa mawe hayo, yana vitu vya thamani ndani yake jambo ambalo siyo la kweli.
“Tunakubalina na viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kutengeneza na
kurejesha mawe ambayo yameng’olewa ila katika hili pia wananchi
tutawaelimisha na kuwashirikisha katika kulinda mipaka yetu kwani
kumekuwa na baadhi ya watu ambao wanachimba mawe yaliyopo katika
mipaka, na kutengeneza matofali, jambo ambalo ni kinyume na
sheria,” alisema Ole Medeye
Alisema Wizara ya ardhi itashirikiana na uongozi huo wa mkoa, kuzuia vitendo hivyo vya uchimbaji katika maeneo ya mipaka, kwani kwa mujibu wa sheria Wizara ya nishati na madini hairuhusiwi kutoa leseni kwa ajili ya shughuli za uchimbaji katika mipaka.
“Dhumuni la ziara hii lilikuwa ni kuhakiki usalama wa mawe yaliyowekwa
mipakani na kuona kama kuna uvamizi wa maeneo ya mipaka kwani jukumu la kupima, kusimamia na kutunza mipaka ya kimataifa baina ya Tanzania na jirani zake ni la Wizara ya ardhi, hivyo lazima tuhakikishe mipaka inalindwa,” akimalizia Ole Medeye
Kwa upande wake Kamishna msaidizi wa ardhi Kanda ya Kaskazini, Doroth Wanzalla akizungumza katika eneo hilo alisema kuwa wananchi wanaojishughulisha na shughuli zozote katika mipaka. Kamishna huyo anasema kuwa kwa mujibu wa sheria za upimaji na ramani ni marufuku kung’oa mawe yaliyowekwa katika mipaka.
“Huo ni uharibifu wa mali za Serikali, ila kwa yeyote atakayebainika
kuhujumi miundombinu hiyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi
yake,” aliongeza Wanzalla.