ALIYEKUWA Meneja wa Kampeni za Urais wa CUF mwaka 2010, Said Miraji na wenzake jana waliwasilisha rasmi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa maombi ya usajili wa muda wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC).
Juzi, Miraji na aliyekuwa mgombea ubunge wa Temeke kwa tiketi ya CUF, Adawi Limbu walijitoa chama hicho na kutangaza kusudio la kusajili chama kipya.
Jana, ujumbe wa chama hicho uliwasili katika Ofisi ya Msajili, Dar es Salaam saa 7:30 mchana ukiongozwa na Miraji ambaye alijitangaza kuwa ni Kaimu Mwenyekiti na Katibu Mkuu wake, Limbu na kupokewa na Wangalizi wa Ofisi ya Msajili, Galasia Simbachawene.
Akizungumza na viongozi hao, Simbachawene alisema kulingana na taratibu za usajili wa vyama, maombi ya chama kabla ya kuwasilishwa kwa msajili yanahitaji kupatiwa muda ili yapitiwe na maofisa mbalimbali akiwemo Mwanasheria wa Ofisi ya Msajili.
“Nimepokea maombi. Msiwe wasiwasi yameshafika kwa Msajili. Utaratibu uliopo ni kwamba maombi yanapokewa na kupewa muda zaidi wa kuyapitia kwa kushirikiana na mwanasheria ili kuona kama yamekamilika baada ya hapo yatawasilishwa rasmi kwa Msajili,” alisema Simbachawene.
CHANZO: Mwananchi, kusoma habari hii zaidi tembelea:- www.mwananchi.co.tz