Yanga Zamalek kucheza saa 12, Simba kuchezeshwa na Wasomali

Baadhi ya wachezaji wa Yanga ya Dar es Salaam

MECHI ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Zamalek na Yanga itachezwa Machi 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jeshi jijini Cairo kuanzia saa 12 jioni kwa saa za Misri.

Maelekezo haya yametolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na kwamba mechi hiyo itachezwa bila washabiki kwa vile Zamalek inakabiliwa na adhabu ya kucheza mechi hiyo bila washabiki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura; mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Morocco ambao ni Jihed Redouane, Rouani Bouazza na Bekkali Mimoun wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Gihed Greisha wa Misri. Kamishna wa mchezo huo ni Ben Khadiga wa Tunisia.

Wakati huo huo; mwamuzi i Yabarow Hagi Wiish na wasaidizi wake Aweis Ahmed Nur na Abdirahman Omar Abdi, wote kutoka Somalia ndiyo watakaochezesha mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba na Kiyovu Sport ya Rwanda.

Kwa mujibu wa orodha ya waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), mwamuzi wa akiba kati mechi hiyo namba 14 itakayochezwa Machi 4 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam atakuwa Waziri Sheha wa Tanzania. Kamishna wa mechi hiyo ya raundi ya awali atakuwa Jean Marie V. Hicuburundi kutoka Burundi.

CAF imeziingiza moja kwa moja kati raundi ya kwanza timu 16 kutokana na ubora wake. Timu hizo ni ES Setif (Algeria), Interclube (Angola), Asec Mimosas (Ivory Coast), Enppi (Misri), AS Real Bamako (Mali), CO de Bamako (Mali) na CO Meknes (Morocco).

Nyingine ni WAC (Morocco), Warri Wolves (Nigeria), Heartland (Nigeria), St. Eloi Lupopo (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Us Tshinkunku (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), El Amal Otbara (Sudan), Al Ahly Shandy (Sudan), CSS (Tunisia) na CA (Tunisia).