KIFO CHA OSAMA:NDIO HATMA YA DONALD TRUMP KISIASA?

Nilipokiona hichi kikaragosi cha ndugu yetu GADO, niliguswa sana na nikaona sina budi kuandika mawili matatu hapa katika baraza letu la uchambuzi nyeti.  Tajiri la vitega uchumi wa majumba Marekani, Bw. Donald Trump ameumbuka hivi karibuni kutokana na ile hulka yake ya kudadisi na kutilia mashaka uraia wa Rais Obama. Siku za hivi karibuni, Trump amekuwa mstari wa mbele kuwahimiza Wamarekani na vyombo vya habari kumshinikiza Rais Obama aonyeshe cheti chake cha kuzaliwa, ili kuthibitisha kama kweli amezaliwa Marekani.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na mimi binafsi, tuna amini kuwa huu ni mchezo mchavu wa kisiasa, ambao Bw. Trump anautumia, ili kujiongezea umaarufu na kuweza kufanikiwa kuwa mgombea wa urais wa Marekani hapo mwakani 2012. Nasema ni mchezo mchafu wa kisiasa kwa sababu Wamarekani pamoja na Rais Obama wana mambo ya msingi ya kufanya zaidi ya kuonyesha cheti cha kuzaliwa. Binafsi sina shaka kwamba Obama ni mzaliwa wa Marekani, na hivyo basi ni Rais halali wa Marekani. Baada ya kelele za Trump kuongezeka, hivi karibuni Obama alilazimika kujitokeza hadharani na kwa mara nyingine tena kuliongelea suala la uraia wake.

Obama mbali ya kuonyesha cheti chake cha kuzaliwa tena, pia aliwathibitishia wa Marekani kuwa madai ya Trump hayana msingi wowote na yeye kama Rais anayo mambo ya kufanya, ambayo ni ya msingi zaidi. Muda si mrefu baada ya kauli hiyo, tunasikia taarifa za kuvamiwa na kuuwawa kwa Osama Bin Laden, mtu ambaye amekuwa akitafutwa na serikali ya marekani kwa takribani miaka 10, ili kujibu tuhuma za milipuko ya September 11, jijini New York, ambapo takribani maisha ya Wamarekani 3,000 yalipotea.

Kuuwawa kwa Osama Bin Laden kumeleta faraja kubwa kwa Wamarekani, na ghafla tunashuhudia jinsi umaarufu wa kisiasa wa Obama unavyopanda na hivyo kujisafishia njia ya kurudi ‘White House’ hapo mwakani. Je wakati Trump anamchokonoa Obama aonyeshe “cheti cha kuzaliwa” alijua kuwa mwenzie anashughulikia suala hili nyeti kwa Wamarekani wote? Donald Trump sasa hivi anaonekana ni kichekesho tu mbele ya Obama. Kama hicho kikaragosi kinavyoonesha, si ajabu Trump akadai pia aonyeshwe “Death certificate” ya Osama, ili kuthibitisha kama kweli amekufa.

Endapo Trump atafanya hivyo, basi lazima tukumbuke kwamba, hayupo ‘serious’ kuona hicho cheti, bali kuwepo kwenye taarifa za habari mbalimbali na hivyo kujiongezea umaarufu. Trump ni bingwa wa kujitangaza.

By Rungwe Jr.

rungwe@dev.kisakuzi.com