Na Mwandishi Wetu
JAMII za makabila ya Kimasai wanapaswa kutambua kuwa wakisomesha watoto wao wa kike na wa kiume familia zitaendelea kupata chakula na fedha hata kama mabadiliko ya tabia nchi yatasababisha mifugo kufa kutokana na kukosa malisho.
Hivyo wazingatie kuwa endapo itatokea mabadiliko ya tabia nchi kusababisha ukosefu wa malisho ya mifugo, familia zitakazoweza kuendelea na maisha bila shida ni zile tu ambazo watoto wao watakuwa wamesoma na kupata ujuzi wa kuajiriwa au kujiajiri badala ya kutegemea mifugo peke yake.
Wamasai na wafugaji wengine wanapaswa kutambua kuwa mtoto wa kike aliyesoma ana faida kubwa na endelevu kwa familia kuliko ngombe wanaotolewa kama mahari ya ndoa. Baadhi ya Wamasai walioojiwa wamedai kwamba watoto wao wa kike wakisoma wanabadilika na kukataa kuketekwa na kuolewa na wanaume wenye umri mkubwa ambao ndio wana uwezo wa kutoa ng’ombe wengi kama mahari.
Sisi TAMWA tunawapongeza baadhi ya Wamasai ambao wamekuwa na ujasiri na kuacha imani potofu ya kudhani kuwa kumsomesha mtoto wa kike ni hasara kwa wazazi wake eti kwa ataishia kuolewa na hivyo familia ya mume wake ndiyo itanufaika zaidi.
Lakini iko mifano mingi nchi nzima inayoonyesha kuwa familia ziliosomesha watoto wao wa kike zimepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na jinsi watoto hao wanavyosaidia wazazi wao. Tumelazimika kutoa tamko hili kwa sababu mwaka huu 2012 pekee yameripotiwa matukio karibu kumi kuhusu watoto wa Kimasai wanaokatishwa masomo ili waolewe kwa mahari yang’ombe.
Njama hizo ni pamoja kuwashawishi watoto wao waandike majibu yasiyofaa kwenye mitihani ili wafeli wasiendelee na shule waolewe. Matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni yalionyesha kuwa baadhi ya watoto waliofeli walikuwa wameandika au kuchora vitu vya hovyo kwenye makaratasi ya mitihani badala ya kujibu maswali waliyoulizwa.
Tunawaomba walimu wa shule zote za msingi na sekondari nchini kuhakikisha kuwa wanajiepusha na vishawishi kutoka kwa wazazi ambao wana malengo maovu ya kuwakatisha watoto wa shule masomo ili waolewe. Tunaamini kuwa walimu wakishirikiana vema na wazazi, kutaepusha watoto wengi wa kike kukatisha masomo ili kuolewa au kupata ujauzito na badala yake watoto hao watafanikiwa kusoma na kufaulu.