*40 pekee watakiwa kwenda uwanjani
Na Mwandishi Wetu
MSAFARA wa Yanga utakaokuwa uwanjani kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek itakayochezwa wikiendi ijayo nchini Misri unatakiwa kuwa na watu wasiozidi 40.
Kwa mujibu wa maelekezo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) yaliyotumwa jana Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ni idadi hiyo tu inayotakiwa kwa vile Zamalek inakabiliwa na adhabu ya kucheza mechi hiyo bila washabiki.
Adhabu ya Zamalek kutocheza mechi mbili za nyumbani za michuano hiyo bila washabiki ilitolewa Aprili 20 mwaka jana na Bodi ya Nidhamu ya CAF iliyokutana jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Mechi dhidi ya Yanga ndiyo itakayokuwa ya kwanza kwa Zamalek kuanza kutumikia adhabu hiyo iliyotakana na washabiki wake kufanya fujo kwenye mechi ya michuano hiyo mwaka jana ilipocheza dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
Hivyo kila timu (Yanga na Zamalek) katika mechi hiyo inatakiwa kuwa na wachezaji ambao wana leseni za CAF kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa 2012. Pia benchi la ufundi katika kila timu linatakiwa kuwa na watu watano.
Kwa klabu zote mbili, kila moja imeruhusiwa kuingia na wajumbe wake wa Kamati ya Utendaji wasiozidi kumi. Mbali ya klabu hizo mbili, wengine waliotajwa kuruhusiwa kuingia uwanjani ni vijana 20 watakaofanya kazi ya kuokota mipira (ball-boys).
Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Morocco ambao ni Jihed Redouane, Rouani Bouazza na Bekkali Mimoun wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Gihed Greisha wa Misri. Kamishna wa mchezo huo ni Ben Khadiga wa Tunisia.