Wanaharakati wavionya vyombo vya dola!

Baadhi ya wanaharakati wakizungumza na vyombo vya habari

SISI wanachama wa Muungano wa Wanaharakati tunaotetea usawa wa kijinsia, haki za binadamu na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FemAct) nchini Tanzania tunaojumuisha zaidi ya asasi za kiraia zipatazo 40 tumechukizwa na tendo la kukamatwa kwa wanaharakati 16 tarehe 9 Februari 2012 jijini Dar es Salaam na kufunguliwa mashtaka eti kwa kosa la kufanya mkusanyiko haramu.

Miongoni mwa waliokamatwa ni wafanyakazi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mkurugenzi Mtendaji, Dk. Helen Kijo-Bisimba, Anna Migila, Marcus Albany na Godfrey Mpandikizi; Ananilea Nkya, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi Habari Wanawake Tanzania (TAMWA); Irenei Kiria, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la SIKIKA; wafanyakazi na wanachama wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wakiwemo Dk. Diana Mwiru, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia, Anna Kikwa, Mkuu wa Idara, Utawala na Fedha na Dorothy Mbilinyi, Afisa Mwandamizi wa Programu, Ukuzaji wa Mitaala na Mafunzo, Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia; wajumbe kutoka vikundi na mitandao ya kijamii, wakiwemo: Specioza Mwankina, kutoka Mtandao wa Watu wenye Ulemavu washio na VVU (NEDPHA); Esther Tibaigana kutoka Kikundi cha Wanawake cha Tushikamane; Janeth Mawinza wa Kikundi cha Wanawake cha Jipange na Mwanaidi Mkwanda kutoka kikundi cha Community Care.

Wanaharakati hawa walikamatwa wakiwa wanaelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kusubiri hatma ya mazungumzo kati ya Waziri Mkuu na madaktari kutoka hospitali za umma ambao kwa majuma kadhaa walikuwa katika mgomo wa kushinikiza madai yao ya muda mrefu. Siku moja tu kabla ya kukamatwa zaidi ya wanaharakati 200 wakiwemo waliokamatwa waliandamana kwa amani kupinga ukimya mrefu wa serikali ambapo mamia ya Watanzania wakipoteza maisha kwa kukosa haki yao ya kupata huduma za afya stahili kwa vile serikali imekosa kuingilia kati na kutatua madai ya madaktari.

Maandamano hayo yaliyoitishwa kwa ushirikiano wa FemAct, Jukwaa la Katiba, Policy Forum, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na asasi nyinginezo yalimulikwa vyema na vyombo vya habari kwa vile yalifanyika kwenye barabara inayotumiwa na wanasiasa wengi pamoja na viongozi wa serikali na kusababisha msongamano wa takriban masaa mawili.

Hakika mashtaka dhidi ya wanaharakati ni haramu na ya kukemewa hasa ukizingatia kuwa wanaharakati hao walikuwa wakitekeleza haki yao ya kikatiba ya kujieleza (Ibara ya 18); na pia wakilinda haki ya kuishi ya Watanzania wenzao (Ibara ya 14) ambao walinyimwa huduma za dharura na za kuokoa maisha yao. Sisi, tulioweka sahihi yetu hapo chini, kwa pamoja tunaeleza kutofurahishwa kwetu na vitendo na hatua za Jeshi la Polisi na serikali kwa ujumla kwa namna walivyolishughulikia suala hili.

Tafadhali andika, piga simu au tuma ujumbe wa barua pepe kwa:
i) Waziri Mkuu: Simu: +255 22 2111249/50/51/52; Faksi: +255 22 2117266; Barua pepe: ps@pmo.go.tz;
Website: http://www.pmo.go.tz;
ii) Inspekta Jenerali wa Polisi: Simu: +255 22 2113461; Faksi: +255 22 2136556; Barua pepe: phq@policeforce.go.tz; Website: www.police.go.tz
iii) Mkurugenzi wa Mashtaka: Simu: +255 22 2113626/2133315
iv) Waziri wa Sheria na Masuala ya Kikatiba: Simu: +255 22 2137833, Faksi: +255 22 2137831, Barua pepe: katibumkuu@sheria.go.tz;
v) Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai(RCO): Simu: +255 (784) (0754) (0777) (0713) 377 425
vi) Wizara ya Mambo ya Ndani Simu: +255 22 2119050 au +255 – 22- 2112036 au +255 – 22- 2112040; Faksi: +255 – 22- 2119050; Barua pepe: ps@moha.go.tz, ps@moha.go.tz

Na kuwataka:
1. Kuacha mara moja hatua zozote za kuwashtaki waliokamatwa na kushtakiwa kwao dhidi ya kuandamana kupinga kutowajibika kwa serikali.

2. Kuwa serikali ya Tanzania na taasisi zake iache kuwanyanyasa kwa namna yoyote ile wananchi wanaodai na kushinikiza kupata haki zao kwani kufanya hivi ni kinyume na misingi ya demokrasia na kanuni za kikatiba zinazotukuza uhuru na haki za binadamu; na

3. Serikali ya Tanzania iwaombe radhi wananchi wake kwa kuhatarisha uhai na afya zao kwa kukosa kuwajibika na kwa kukosa kuwatimizia wafanyakazi wake haki zao.

Imetolewa na FemAct na kusainiwa na:
Usu Mallya
Mkurugenzi Mtendaji
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Sekretarieti ya FemAct