Na Mwandishi Wetu, Arusha
SHAHIDI wa saba katika kesi ya kupinga matokeo ya Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA), Joseph Silvester, amedaiwa kutoa
ushahidi aliousikia mitaani badala ya ushahidi aliousikia kwenye
mkutano.
Madai hayo yalitolewa na wakili wa mdaiwa wa kwanza Lema, Method
Kimomogoro, wakati akimhoji shahidi huyo katika mbele ya Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Sumbawanga ambaye anasikiliza kesi hiyo katika
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Kimomogoro alitaka kujua iwapo maneno aliyotoa shahidi huyo akidai
kwamba yalitamkwa na Lema katika mkutano uliokuwa umefanyika uwanja wa
Big Sister, kata ya Olorien, mkoani hapa dhidi ya aliyekuwa mgombea wa
CCM, Dk. Batilda Burian, alikuwa ameyasikia yakitamkwa la Lema au la.
Mahojiano kati ya wakili Kimomogoro na shahidi Joseph yalikuwa kama ifuatavyo;
Wakili: Uliwahi kuhudhuria mikutano ya kampeni ya uchaguzi ya Dk. Batilda?
Shahidi: Hapana
Wakili: Ni kweli watu wakitoka kwenye mikutano ya kampeni za uchaguzi
walikuwa wanajadili yaliyojiri kwenye mikutano hiyo, siyo?
Shahidi: Ndiyo
Wakili: Nikikuambia haya maneno yanayodaiwa kutolewa na Lema yalikuwa
yamezungumzwa kwenye mikutano yote, wewe umeyaookota mitaani, siyo?
Shahidi: Sijayaookota mitaani.
Wakili: Unamfahamu Dk. Batilda?
Shahidi: Simfahamu
Wakili: Hadi leo?
Shahidi: Ndio
Wakili: Ni nani alikuambia unahitajika kuja kutoa ushahidi
Shahidi: Ni Agness Mollel (PW2)
Wakili: Uliwahi kuhudhuria mkutano wa kampeni wa aliyekuwa mgombea
ubunge kupitia CCM,Dk. Batilda?
Shahidi: Hapana
Wakili: Ni kweli watu wanapotoka kwenye mkutano wa hadhara ya kampeni,
hujadili mambo yaliyojiri kwenye mkutano huo?
Shahidi: Ndiyo
Wakili: Ni kweli kwamba wananchi walikuwa wakijadili yaliyojiri kwenye
mikutano yote ya kampeni?
Shahidi: Ndio
Wakili: Nikikuambia hayo maneno unayodai yametamkwa na Lema dhidi ya
Dk. Batilda, kuwa yalikuwa yamezungumzwa kwenye mikutano ya CCM ambapo
yalikuwa ni maswali aliyokuwa anaulizwa Batilda na wana CCM wenzake,
na wewe umeyaokota mitaani?
Shahidi: Sijayaokota mitaani
Wakili: Ulipotoka kwenye mkutano huo uliwahi kuripoti juu ya hayo
maneno unayodai ameyasema Lema dhidi ya Dk. Batilda?
Shahidi: Sijawahi kuripoti mahali po pote
Wakili: Hata kwa afisa mtendaji wako?
Shahidi: Sijawahi kumwambia
Wakili: Hayo maneno unayosema Lema alisema kwenye mkutano unafahamu
kwamba ni maneno ambayo Dk. Batilda alikuwa anaulizwa?
Shahidi: Sifahamu
Wakili: Uliwahi kuhudhuria mikutano ya Dk. Batilda?
Shahidi: Hapana
Awali shahidi huyo akiongozwa na wakili wa upande wa wadai katika kesi
hiyo Modest Akida, mahojiano yao yalikuwa kama ifuatavyo;
Wakili: Ulihudhuria mikutano gani?
Shahidi: Chadema, CCM na TLP
Wakili: Mkutano wa Chadema uliohudhuria ulifanyika wapi?
Shahidi: Uwanja wa Bigsister, Septemba 1 mwaka 2010, kuanzia saa 10 jioni
Wakili: ulipofika katika mkutano huo kitu gani kilikuwa kinaendelea?
Shahidi: Walikuwa wanamsubiri mgombea(Lema)ambaye alifika saa 10
Wakili: alipofika nini kiliendelea?
Shahidi: Alisalimia ‘peoples halafu watu wakaitikia Power’
Wakili: Baada ya salamu hiyo nini kiliendelea?
Shahidi: Alianza kujinadi
Wakili: Alijinadije?
Shahidi: Alianza na kero ya ulinzi shirikishi katika kata ya Olorien
Wakili: alisemaje?
Shahidi: Wananchi wanakamatwa na kutozwa fedha za ulinzi shirikishi
Wakili: Akasemaje tena?
Shahidi: alisema akichaguliwa atawapunguzia kodi ya magari (daladala)
Wakili: Mambo mengine?
Shahidi: Asichaguliwe Dk. Batilda kwa sababu ameolewa na Mzanzibar
Wakili: Akasemaje tena?
Shahidi: Na hapo alipo ana mimba ya fisadi Lowassa
Wakili: alisema jambo lolote tena
Shahidi: Alisema mkimchagua Dk. Batilda atafunga redio Safina,atajenga
Msikiti mkubwa
Wakili: Jambo lingine?
Shahidi: Mkimchagua Dk. Batilda badala ya kuwawakilisha Bungeni atakuwa
“Maternity” Zanzibar
Juzi shahidi huyo aliwekewa pingamizi na Wakili Kimomogoro, baada ya
kuieleza mahakama kuwa wakati shahidi wa pili(Agness Mollel na shahidi
wa nne Musa Mpamba ambaye ni Katibu wa CCM wilaya ya Kyela wanatoa
ushahidi wao mahakamani hapo, shahidi huyo wa saba alikuwepo hivyo
aliiolmba mahakama kutokupokea ushahidi wa shahidi huyo.
Jaji anayesikiliza kesi hiyo Jaji mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya
Sumbawanga Gabriel Rwakibarila, aliruhusu shahidi huyo kutoa ushahidi
na iwapo ushahidi wake utaonekana kufanana na ushahidi uliotolewa na
shahidi wa pili na wa nne, utaachwa.
Awali akihojiwa na wakili wa wadai, Joseph aliieleza mahakama kuwa
hakuwepo siku mashahidi hao walipokuwa wanatoa ushahidi wao (Februari
13 na 15) kwani alikuwa amepata ajali ya pikipiki tarehe 11, na kulala
nyumbani kwa siku tano.
Hata hivyo Kimomogoro alitaka kujua iwapo shahidi huyo anayo fomu
namba 3, inayotolewa na polisi(PF3), naye akajibu hana na wala
hakuripoti polisi kuhusu ajali hiyo.
“Ahhaaaa mwalifu mkubwa wewe, hujui kama ni kosa, kutokuripoti ajali
polisi” alihoji Kimomogoro Shahidi alijibu hajui na Kimomogoro akamweleza kuwa kumbe maneno ya kwenye mkutano unayajua. Jaji huyo aliahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu ya wiki ijayo, ambapo shahidi wa nane atatoa ushahidi wake.