Viingilio Stars na Msumbiji

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah

KIINGILIO cha chini katika mechi ya mchujo ya Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Msumbiji (Mambas) itakayochezwa Februari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 3,000.

Jumla viti 36,693 (rangi ya bluu na kijani) ndivyo vitakavyotumika kwa kiingilio hicho katika uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 wakiwa wameketi.

Viingilio vingine ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C, sh. 15,000 kwa VIP B wakati kwa watakaokuwa miongoni mwa watakaokaa katika viti VIP A ambavyo viko 748 tu watalazimika kulipa sh. 20,000 kwa kila mmoja.

Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha mafuta cha Bigbon kilichopo Msimbazi (Kariakoo), mgahawa wa Steers ulioko Barabara ya Samora/Ohio, Kituo cha mafuta cha Oilcom Ubungo na Uwanja wa Taifa.

Wakati huo huo; mkoa unaotaka kuwa mwenyeji wa fainali za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zinazoshirikisha timu tisa bora za ligi hiyo unatakiwa kutoa sh. milioni 25 ambazo ni gharama za kuendesha fainali hizo.

Haki ya kuwa mwenyeji wa fainali hizo iko wazi kwa mikoa yote wanachama wa TFF ingawa tayari ipo minne ambayo imeshatuma rasmi maombi ya kuandaa fainali hizo. Mikoa hiyo ni Mbeya, Mwanza, Ruvuma na Tabora.

Kwa mikoa ambayo itakuwa tayari kuwa mwenyeji kwa maana ya kutimiza sharti hilo la kutoa kiasi hicho cha fedha inatakiwa iwe imefanya hivyo kufikia Machi 15 mwaka huu. Pia kumefanyika mabadiliko ya kuanza fainali hizo, sasa zitaanza Machi 31 mwaka huu badala ya Machi 17 ambayo ilitangazwa awali.

Wakati huo huo; pambano la kirafiki la kimataifa kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC (Leopards) lililofanyika Februari 23 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 32,229,000. Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 11,420 waliokata tiketi kushuhudia mechi kwa kiingilio cha sh. 2,000, sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000 na sh. 15,000.

Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 5,916,288, gharama ya kuchapa tiketi sh. 2,250,000, malipo kwa kamishna wa mchezo sh. 150,000, malipo kwa waamuzi wanne sh. 480,000, ulinzi na usafi kwa Uwanja wa Taifa sh. 2,350,000, Wachina sh. 2,000,000, umeme sh. 300,000 na maandalizi ya uwanja (pitch marking) sh. 400,000.

Nyingine ni asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 3,676,542, asilimia 10 ya uwanja sh. 1,838,271, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 919,136 na asilimia 65 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 11,948,763.