MKUTANO wa kimataifa kuhusu hatma ya Somalia umemalizika mjini London kwa Serikali ya Uingereza pamoja na Marekani zikisisitiza nchi hiyo lazima isaidiwe kusimama tena na kuwa nchi thabiti na yenye amani.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, akifunga mkutano huo amesema yalioafikiwa katika mkutano huo ni jinsi ya kumaliza uharamia, kutoa misaada ya kibinadamu, usalama na kulitokomeza kundi la Al Shabaab.
Nayo Marekani imetishia kumuwekea vikwazo yeyote atakayekwamisha mageuzi ya kuijenga upya Somalia. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron aliusifu mkutano huo na kuutaja kama nafasi pekee ya kuigeuza Somalia na kuifanya thabiti na yenye mafanikio makuu.
“Mauritius, Tanzania na Usheli sheli zimekubali kuwapokea washukiwa wote wa uharamia na kuwafungulia mshitaka nchini humo. Somaliland na Puntland na zimekubali kuwapokea na kuwaweka gerezani maharamia wote ambayo tayari wamehukumiwa vifungo katika mahakama mbali mbali duniani. Maharamia wote hawatahurumiwa, wafadhili wao vile vile hawatahurumiwa. Pia tumekubaliana kuhusu kuundwa kwa jopo kazi kuhusu kuzuia ulipaji wa vikombozi kwa maharamia na pia kuzuia uharamia usionekane kama kazi inayoleta utajiri wa haraka haraka,” Waziri Mkuu alisema.
Amesema kama hatua ya kuisaidia Somalia, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimejitolea kuwapokea maharamia wote wa Kisomali watakao kamatwa na kisha kuwashitaki katika Mahakama za Dar es Salaam.
David Cameron amesema hatua hii ina lengo la kuwabana kabisa maharamia.
Lakini waziri huyo mkuu amesema kuwa njia muhimu zaidi ya kuisaidia Somalia ni kuhakikisha kuna uthabiti wa kisiasa. Katika mkutano huo ambao kundi la Al shabaab halikualikwa uliapa kukabiliana na kundi hilo na washirika wake wote.
Waziri wa Masuala ya nchi za nje wa Marekani, Hilarry Clinton alitangaza kuwa nchi yake haitashirikiana na magaidi na hata makundi ya wanamgambo walioko Somalia.
Hata hivyo kabla ya mkutano huo wa London kuanza msemaji wa Al Shabaab Sheikh Ali Rage aliupuuza mkutano huo na kutoa onyo kwa Uingereza, kutoingilia masuala ya ndani ya Wasomali.
-BBC