Taifa Stars na DRC Congo hakuna mbabe!

Mchezaji Ilunga (kushoto) wa Jamhuri ya Kiodemokrasia ya Congo akichuana na mchezaji Hussein Javu wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) wakati wa mchezo wao wa kirafiki uliofanyika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam. (Picha na Fullshangwe Blog)

Na Mwandishi Wetu

TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) jana ilishindwa kuonesha cheche za kucheza katika uwanja wa nyumbani (Uwanja wa Taifa Dar es Salaam) baada ya kutoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa kirafiki na Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kiodemokrasia ya Congo-DRC.

Mchezo huo ulikuwa ni kwa ajili ya kujipima nguvu kabla ya mapambano ya timu hizo kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini, ambapo Taifa Stars itakutana na Msumbiji na RDC Congo itapepetana na Sychelies.

Katika mchezo huo Kocha Mkuu wa Taifa Stars alichezesha wachezaji wake wote wanaounda kikosi cha timu ya taifa, baada ya nusu ya kwanza kuchezesha wachezaji kikosi kizima kisha baada ya mapumziko kuingiza tena kikosi kingine tofauti na mwanzo.

Wachambuzi wa soka walisema kocha huyo aliamua kufanya hivyo ili kutafuta kikosi cha kwanza ambacho hadi sasa bado ajakipata kutokana na viwango vya wachezaji kubadilika mara kwa mara hasa kushuka.