Mbunge Nyika aishauri Dawasco

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika

BODI ya wakurugenzi ya DAWASCO chini ya uenyekiti wa Mhandisi Suleiman Said Suleiman na Mtendaji Mkuu wa kampuni Jackson Midala wanapaswa kurekebisha kwa haraka mfumo mzima wa ufuatiliaji wa DAWASCO kuwezesha ukaguzi wa ufanisi wa mtandao mzima wa maji.

Katika kipindi hiki cha matatizo makubwa ya maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ikiwemo katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo DAWASCO iache kuwatumia wafanyakazi wanaohusika na ukaguzi kufanya kazi tofauti za kusoma mita na kugawa Ankara badala yake wafanyakazi tajwa wafanye ufuatiliaji wa dharura wa ufanisi wa mtandao mzima wa maji katika maeneo mbalimbali.

Baadhi ya maeneo ambayo yanapaswa kutembelewa ni kata za Makuburi, Kimara, Saranga, Mbezi Luis, Msigani, Kwembe, Goba, Kibamba, Sinza, Makurumla, Mabibo, Manzese, Ubungo na Mburahati.

Kwa upande mwingine, kwa kuwa mkataba wa huduma kwa wateja unatoa haki kwa wateja wa DAWASCO lakini pia unaeleza wajibu; natoa mwito kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam kutimiza wajibu wa kuwaelekeza wakaguzi husika mitaa yenye matatizo katika mtandao wa maji ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Mkataba huo unawataka wateja wa DAWASCO kutoa taarifa kuhusu uharibifu wa miundombinu, wizi wa maji na kuhusu matatizo ya maji hivyo wananchi watoe taarifa husika na kufuatilia wakaguzi kufika maeneo yao kwa kupiga nambari ya bure 0225500240 au 0762979627 za DAWASCO makao makuu.

Pia, wananchi wanaweza kuwasilisha kero za maji kwa ofisi ya DAWASCO zilizo katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam na kupitia nambari zifuatazo: Temeke +255 775016184, Ilala +255 775048556, Magomeni +255 775016179, Boko/Tegeta +255 775048553, Tabata +255 775016181, Kawe +255 775016185, Kinondoni +255 775016180 na Kimara +255 775048554.

Wananchi watumie pia nafasi hii kuwasilisha kwa DAWASCO maelezo na vielelezo kuhusu maeneo ambayo hakuna miundombinu ya maji kabisa au miundombinu iliyopo haijawahi kutoa maji kwa kipindi kirefu kwa ajili ya kutaka hatua za ziada.
Matatizo ya maji katika maeneo mengi ya jiji la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo yamedumu kwa miaka mingi, wananchi wametupa wajibu wa kuwawakilisha kuisimamia serikali na mamlaka zake kupunguza kero husika kwa haraka hivyo wananchi watarajie vitendo zaidi vya kushinikiza uwajibikaji kwenye sekta ya maji katika kipindi cha karibuni.