Hamad Rashid aiwekea CUF pingamizi

Mh. Hamad Rashid

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed na wenzake 10, wamewasilisha Mahakama Kuu mapingamizi ya kisheria, wakidai kiapo kilichowasilishwa na Wakili Twaha Taslima anayewawakilisha wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF) katika kesi dhidi ya wadhamini hao, kina upungufu wa kisheria.

Kiapo hicho cha Taslima kinajibu hoja ya Hamad na wenzake kuhusu maombi madogo katika kesi ya msingi waliyoyawasilisha mahakamani hapo dhidi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF, akiwamo Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Hati ya mapingamizi hayo iliyowasilishwa mahakamani hapo na wakili anayemwakilisha Hamad na wenzake katika kesi hiyo, Augustino Kusalika, imedai upungufu mmojawapo uliomo kwenye kiapo hicho cha Taslima, ni pamoja na kuweka masuala ya kisheria kwenye kiapo.

Upungufu wa mwingine, hati hiyo inadai kuwa ni Taslima kutokutaja chanzo cha habari kilichomueleza mambo aliyoyaeleza kwenye kiapo hicho.

Hamad na wenzake, wanaiomba mahakama iwaamuru wajumbe hao wa Baraza Kuu kufika mahakamani kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua, ikiwamo kufungwa jela kwa kukiuka amri halali ya mahakama.

Amri hiyo ya mahakama ilizuia kufanyika kwa mkutano wa Baraza Kuu, Januari 4, mwaka huu, Zanzibar, hadi hapo kesi ya msingi iliyofunguliwa na Hamad na wenzake itakapoamuliwa na mahakama. Hata hivyo, mkutano huo ulifanyika ambapo pamoja na mambo mengine, uliwavua uanachama Hamad na wenzake.

Katika kiapo chake, Taslima pamoja na mambo mengine, anamtaka Hamad na wenzake kuthibitisha amri hiyo ya mahakama inayodaiwa kuwa ilipelekwa katika ofisi za CUF, Buguruni, jijini Dar es Salaam, Januari 4, mwaka huu na kukataliwa kupokelewa, kama kweli iliwafikia wajumbe hao wa Baraza Kuu kwa wakati, kama walivyodai katika hati yao ya maombi.

Wakati huo huo, kesi ya mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila na wenzake, imeahirishwa hadi Machi 15, mwaka huu.

Kesi hiyo inayowakabili wadhamini wa Chama cha NCCR-Mageuzi, iliahirishwa jana na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Amir Msumi, kutokana na jaji anayeisikiliza, Alice Chinguile, kuwapo safarini.

CHANZO: NIPASHE