Kesi ya maandamano yashindwa kusikilizwa Arusha

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa

Na Mwandishi Wetu, Arusha

KESI inayowakabili viongozi wa juu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kufanya mkusanyiko na maandamano bila idhini ya vyombo husika leo imeshindwa kusikilizwa kutokana na kuendelea kwa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi 2010, inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema.

Wakili wa utetezi, Method Kimomogoro leo amemuomba Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Arusha, Charles Magesa kuahirisha shauri hilo na kupanga tarehe nyingine ya kusikilizwa kutokana na wakili huyo kwenda katika kesi nyingine inayomkabili Mbunge Lema.

Katika kesi ya kufanya kusanyiko na maandamano pasipo kibali, Lema ni mmoja wa washitakiwa, ambapo upande wa jamhuri ulikuwa tayari umeandaa mashahidi wa tatu kwa ajili ya kuendelea kwa kesi.

Kimomogoro aliieleza Mahakama kutokana na kesi hiyo kuendelea Mahakama Kuu, wana ushahidi wa kufuatilia ambapo Jaji anayesikiliza shauri hilo kuwataka upande huo wa wadaiwa kutoa ushahidi wao pale, upande wa wadai watakapomaliza kutoa ushahidi.

“Kifungu cha 196-197, ya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, kinasema mshitakiwa anapaswa kuwa mahakamani wakati ushahidi dhidi yake unatolewa, na kesi ile ya uchaguzi ina ukomo hadi Mei 30 inatakiwa iwe imemalizwa kusikilizwa,” aliongeza Kimomogoro

Kwa upande wake wakili wa Serikali Edwin Kakolaki aliieleza mahakama hiyo kuwa hoja ilizotolewa na Kimomogoro juu ya kuahirishwa kwa shauri hilo haina msingi kwani shauri hilo lina mawakili watatu wa utetezi, hivyo kutokuwepo kwake hakuzuii shauri hilo kutokuendelea.

“Tunaiomba mahakama hii kutambua umuhimu wa shauri hili kuendelea, pengine washitakiwa waseme hawana imani na mawakili wawili waliosalia, Lema aendelee na kesi ya uchaguzi mahakama kuu, katika kesi hii awakilishwe na mawakili hao,” alisema Kakolaki

Aidha Kimomogoro aliiomba mahakama kupatiwa nakala ya hati ya mashitaka ambayo ina kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kwani katika nakala waliyopatiwa haioneshi kibali cha DPP katika shitaka la 10 na la 11 yanayowakabili Dk. Slaa na Ndesamburo.

Kakolaki alidai licha ya hati hiyo kufanyiwa marekebisho, shitaka la 10 na 11 halijafanyiwa marekebisho na katika hati iliyopita DPP alitoa kibali chenye sahihi yake ya Machi 21, 2011.

“Nadhani wakili mwenzangu ameshindwa kuelewa kwani hati hii siyo mpya bali ni hati ya mashitaka iliyofanyiwa marekebisho katika baadhi ya mashitaka ila shitaka la 10 na la 11 halikufanyiwa marekebisho, hivyo hakuna mahitaji ya kuomba kibali cha Mkurugenzi wa mashitaka tena,” alisema Kakolaki

“Shauri hili linarudi kwa washitakiwa wote, kama wanaridhika kuwakilishwa na wakili wao mmoja au wakiona wanataka kuwakilishwa na mawakili wote wawili, mahakama itasikiliza kwa sababu suala hilo ni haki ya mshitakiwa,”

Magesa alilazimika kuwahoji washitakiwa hao, iwapo wanaridhia shauri hilo liendelee wakiwa wanatetewa na wakili mmoja (Albert Msando) au wanataka mawakili wote, ambapo washitakiwa wote waliieleza mahakama kuwa haafikiani na kutetewa na wakili mmoja bali watanata kutetewa na mawakili wao wote wawili.

“Tuipe mwezi mmoja kama kesi hiyo itakuwa imeisha,tutaendelea na kesi hii na iwapo baada ya mwezi kama haitakuwa imeisha tunaipangia tarehe nyingine ya kuisikiliza kufuatana na mwenendo wa shauri hili utakavyokuwa,” alisema Magesa.

Washitakiwa ni Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, mkewe Josephine Mshumbusi pamoja na Aquiline Chuwa. Hata hivyo Hakimu Magesa amehairisha shauri hilo hadi Machi 28, 2012. Watuhumiwa wengine katika shauri hilo ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi ya upinzani bungeni Freeman Mbowe, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, Derick Magoma, John Materu, Peter Marua, Mathias Valerian, Dadi Igogo, Nai Steven, Walter Mushi, Daniel Titus, Juma Samweli, Richard Mtui, Basil Lema.