Hali si shwari Songea, takribani 16 wadaiwa kuuwawa kikatili, wanyofolewa sehemu za siri

Baadhi ya wananchi wa Songea wakiwa wamenzunguka kuangalia moja ya maiti zilizotelekezwa baada ya kuuwawa kikatili usiku wa kuamkia leo eneo la Mji Mwema.


Maiti iliyouwawa kikatitil eneo la Mji Mwema Darajani ikiwa imetelekezwa kwenye maji, jina la marehemu halikuweza kupatikana mara moja.

Na Mwandishi wa dev.kisakuzi.com, Songea

HALI ya usalama kwa sasa ni tete katika Manispaa ya Songea kutokana na mauaji ya kikatili ambayo yanaendelea kutokea mfululizo katika mji huo. Hadi sasa takribani watu 16 wameripotiwa kuuwawa kikatili na maiti zao kukutwa zimenyofolewa baadhi ya viongo hasa vya siri.

Usiku wa kuamkia leo maiti nne zimeokotwa Manispaa ya Songea maeneo ya Paranyati, Majengo, Matarawe na Mji Mwema, huku zote zikiwa zimeuwawa na kutelekezwa ikiwa ni pamoja na kunyofolewa baadhi ya viungo vya mwili hasa sehemu za siri.

Mauaji hayo yana husishwa zaidi na imani za kishirikikina na watu hao huuwawa kikatili na kundi la watu wasiojulikana, kisha kuchukua viungo vya sehemu za siri (yaani nyeti) kama uume na uke, moyo na koromeo.

Shuhuda mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Jerome Komba akizungumza na dev.kisakuzi.com leo amesema inadaiwa watu hao huchukuwa viungo hivyo na kuvipeleka nchini Msumbiji kwa ajili ya masuala ya uchimbaji madini pamoja na machimbo ya madini ya uraniamu eneo la Namtumbo.

“Yaani ndugu mwandishi hawa watu wanataka utajiri wa haraka haraka na haya madini tuliyo nayo katika mkoa huu (Ruvuma) yata tuponza,” anasema Komba.

Hadi sasa ni wiki ya pili tokea matukio mfululizo yatokee. Kamanda wa Jeshi la Police Mkoa wa Ruvuma, SSP-Naftari Matamba amekiri kutokea kwa matukio hayo katika Mkoa wake hususani, Wilaya ya Songea na amedai polisi wanaendelea na uchunguzi ili kuhakikisha watu wanaojihusisha na vitendo hivyo wanatiwa nguvuni mara moja na kuchukuliwa hatua.
Taarifa zaidi zinadai Jeshi la Polisi Wilayani Songea limewapiga risasi na kuwauwa waandamanaji wawili wakiwa wanajitahidi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakitokea maeneo mbalimbali ya wilaya ya Songea kuelekea Hospitali ya Wilaya na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kupinga matukio ya mauaji ya kikatili ambayo inadaiwa hakuna hatua zinazochukuliwa kwa vyombo vya dola.

Thehabari.com (www.thehabari.com) itakuletea maelezo zaidi ya mauaji haya muda si mrefu.