Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Bibi Amina Saidi Mrisho kuwa Kamishna wa Sensa ya Mwaka 2012. Aidha, Rais Kikwete amemteua Bibi Seraphia Mgembe kuwa Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA).
Taarifa iliyotolewa na kutiwa saini Dar es Salaam Februari 21, 2012, na Kaimu Katibu Kiongozi, Peniel Lyimo imesema kuwa uteuzi huo umeanza Februari 20, mwaka huu, 2012. Taarifa ya Lyimo imesema kuwa kabla ya uteuzi wake, Bibi Amina Mrisho alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Katika taarifa tofauti iliyotolewa na kutiwa saini pia mjini Dar es Salaam Februari 21, 2012, na Katibu Mkuu Ikulu, Peter Ilomo, imesema kuwa uteuzi huo wa Bibi Mgembe umeanza Februari 20, 2012.
Ilomo amesema katika taarifa yake kuwa kabla ya uteuzi wake Bibi Mgembe alikuwa Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa MKURABITA. Bibi Mgembe anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ladislaus Salema ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria.