Kesi ya Mbowe, Dk Slaa yaiva Arusha

Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe

Na Mwandishi Wetu, Arusha

UPANDE wa Jamhuri katika kesi inayowakabili viongozi wa juu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Slaa, kesho unatarajia kutoa ushahidi.

Mahakama pia imewaonya washitakiwa watatu kwa kutofika mahakamani leo na imewataka kesho kufika mahakamani hapo saa 2 asubuhi ili nao wasomewa mashitaka yao baada ya wenzao kusomewa jana. Washitakiwa ambao hawakufika mahakamani leo ni Dk. Slaa, mkewe Josephine Mshumbusi na Aquiline Chuwa.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Arusha, Charles Magessa anayesikiliza shauri hilo, wakili wa utetezi, Albeet Msando ameieleza mahakama hiyo leo kuwa washitakiwa hao wameshindwa kufika mahakamani kutokana na mkanganyiko uliojitokeza. Wakili huyo alidai washitakiwa hao wameshindwa kuja kutokana na mkanganyiko wa tarehe uliojitokeza ambapo wana kesi zaidi ya mbili mahakamani hapo, hivyo hawakukumbuka tarehe sahihi ya kesi ya leo.

“Mheshimiwa kutokana na uzito na umuhimu wa shauri hili na mkanganyiko uliojitokeza kwa baadhi ya washitakiwa, tunaomba washitakiwa waliopo mahakamani leo, wasomewe mashitaka yao na hao ambao hawapo wapangiwe tarehe ya kusomewa mashitaka yanayowakabili na si lengo la upande wa utetezi kuchelewesha shauri hili,” alisema Msando

Kwa upande wake wakili wa Serikali, Edwin Kakolaki, aliieleza mahakama hiyo kuwa madai ya wakili wa utetezi kuwa washitakiwa walipata mkanganyiko kutokana na kuwa na kesi zaidi ya moja, aliiomba mahakama hiyo kuwafutia dhamana washitakiwa hao.

“Mahakama iwafutie dhamana ili wasiweze kupata mkanganyiko tena na hati ya kuwakamata itolewe na kama kesi zinakuwa nyingi mshtakiwa awe na diary ili asisahau, upande wa Jamhuri tumeridhia washitakiwa wengine waliopo mahakamani kusomewa mashitaka yao,” alisema Kakolaki

Wakili huyo akiwasomea mashitaka watuhumiwa hao jana alisema kuwa shitaka la kwanza ambalo linawakabili watuhumiwa wote ni kula njama ya kutenda kosa kinyume cha kifungu cha 385(35) cha kanuni ya adhabu.

Shitaka la pili linalowakabili watuhumiwa wote isipokuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba ni kula njama na kutenda kosa ambapo watuhumiwa hao wanadaiwa kati ya tarehe 3-5 walitenda kosa la kukataa kutii amri halali. Shitaka la tatu linalowakabili watuhumiwa 18 isipokuwa Mwigamba ni kula njama kinyume cha kifungu cha 385(35) ambapo kwa pamoja wanadaiwa kula njama na kufanya kusanyiko lisili halali.

Alidai mahakamani hapo kuwa shitaka la nne linalowakabili washitakiwa 18 isipokuwa Mwigamba ni kula njama na kutenda kosa la kufanya vurugu baada ya katazo la amri halali ya kukatazwa kufanya vurugu.

Alisema kuwa shitaka la tano linalowakabili Dk Slaa na Mbunge wa Moshi Mjini Philemon Ndesamburo, ni kula njama na kutenda kosa la kutoa matamshi yenye kuleta uchochezi. Shitaka la sita linamkabili Dk. Slaa, Ndesamburo na Mwigamba amabo wanashitakiwa kwa kosa la kula njama kwa kuwashawishi watu wengine kufanya kosa.

Shitaka la saba linalowakabili washitakiwa 18, ni kosa la kukataa kutekeleza amri halali kinyume na kifungu cha 42(2) cha sheria ya Jeshi la Polisi na huduma zake, ambapo wanadaiwa kukataa amri halali iliyowaelekeza jinsi ya kufanya maandamano na njia walizopaswa kutumia.

Shitaka la nane dhidi ya washitakiwa 18, ni la kufanya kusanyiko lisilo halali chini ya kifungu cha 45 cha jeshi la polisi, wanadaiwa Januari 5. 2011 eneo la Mt. Meru Hoteli, walikataa amri iliyowataka kutawanyika iliyotolewa chini ya kifungu cha 43(4) cha jeshi la polisi, amri iliyotolewa na Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha, Zuberi Mwombeji.

Shitaka la tisa dhidi ya watuhumiwa 18 ni kufanya fujo baada ya kukataa amri halali ya kutofanya hivyo, ambapo alidai kuwa waliendelea na kusanyiko hata baada ya kupita muda waliokuwa wamepewa na kutokana na tamko lililotolewa na OCD Zuberi la kuwataka kutawanyika.

Shitaka la kumi linamkabili Dk. Slaa ambaye hakuwepo mahakamani ambapo anashitakiwa kwa kutoa matamshi yenye kuleta uchochezi. Shitaka la kumi na moja linamkabili Ndesamburo ambaye anadaiwa kutoa matamshi yaliyokuwa yanakusudia kusababisha uchochezi, anayodaiwa kuyatoa katika viwanja vya NMC.

“Nakwambia Kikwete leo hii umetia saini ya vurugu nchini Tanzania, Polisi Arusha watapiga risasi zitaisha na tutawakamata, Kikwete kama huna baba, Ndesamburo anapigwa na vichanga change vyako, vurugu za Ndesamburo huziwezi sasa tunatekeleza kama tulivyosema” Wakili huyo alimnukuu Ndesamburo, matamshi anayodaiwa kuyatoa.

Shitaka la 12 linalomkabili Slaa, Ndesamburo na Mwigamba la kuwashawishi watu kufanya kosa, ambapo wanadaiwa waliwashawishi wananchi waliokuwa wamekusanyika kufanya kosa la kutaka kuwatoa watu waliokuwa chini ya ulinzi. Shitaka la kumi na tatu linalowakabili watuhumiwa wote ni kufanya fujo kinyume cha kifungu cha 74(3), 76 na 35 vya kanuni za adhabu ambapo wote kwa pamoja wanadaiwa kutekeleza vurugu, kuvunja amani na kusababisha hofu kwa wananchi.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo washitakiwa hao waliyakana mashitaka hayo, ambapo leo saa 3 asubuhi shauri hilo litaendelea kwa upande wa Jamhuri kuleta mashahidi na kuendele kusikilizwa mfululizo hadi Machi mbili.

Hakimu Magesa akiahirisha shauri hilo amewataka watuhumiwa ambao hawakufika mahakamani leo kufika ofisini kesho kwake saa 2 asubuhi ili mahakama ijue wamekuja vinginevyo mahakama utatoa amri ya kukamatwa kwao.

Aidha washitakiwa katika shauri awali walikuwa wanakabiliwa na mashitaka manane (8), ila baada ya hati ya mashitaka kufanyiwa marekebisho, wameongozewa mashitaka hadi kufikia 13. Watuhumiwa wengine katika shauri hilo ni pamoja na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Derick Magoma, John Materu, peter Marua, Mathias Valerian, Dadi Igogo, Nai Steven, Walter Mushi, Daniel Titus, Juma Samweli, Richard Mtui, Basil Lema.