Na Mwandishi Wetu
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Claude Le Roy na msaidizi wake wamewasili nchini jana (Februari 18 mwaka huu) mchana kwa ndege ya Emirates wakitokea Paris, Ufaransa tayari kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Taifa Stars.
Mechi hiyo itafanyika Februari 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mfaransa Le Roy ambaye alianza kuifundisha DRC mwezi Septemba mwaka jana na msaidizi wake wamefikia kwenye hoteli ya Golden Tulip.
Msafara mzima wa timu hiyo wenye watu 24 wakiwemo wachezaji 19 utawasili nchini Jumanne (Februari 21 mwaka huu) na kufikia kwenye hoteli ya Holiday Inn.
Februari 22 mwaka huu (saa 5 asubuhi) kutakuwa na mkutano wa makocha wa timu zote Jan Poulsen (Taifa Stars) na Le Roy (DRC) utakaofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Wakati huo huo, kikosi cha Taifa Stars kilichotangazwa Februari 16 mwaka huu na Kocha Poulsen kesho (Februari 20 mwaka huu) kinaingia kambini jijini Dar es Salaam tayari kwa mechi dhidi ya DRC na ile ya michuano ya AFCON 2013 dhidi ya Msumbiji ambayo itachezwa Februari 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.