Kuoanisha uzito wa magari EAC kutaokoa mamilioni ya dola-Bukuku

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Na James Gashumba, EANA

NCHI wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinaweza kuokoa kiasi cha fedha hadi kufikia dola za Kimarekani bilioni 1.5 kwa mwaka kwa kuoanisha udhibiti wa viwango vya uzito wa magari katika barabara za nchi tano za Jumuiya hiyo.

“Kwa kuanisha viwango vya uzito wa magari hadi kufikia kiasi cha juu kabisa cha tani 56 kwa kila lori linalopita ndani ya kanda, tutaweza kuondoa mzigo wa gharama kwa waendeshaji na wawekezaji katika kanda na kukoa zaidi ya dola za Kimarekani bilioni moja kwa mwaka,” alisema Enos Bukuku, Naibu Katibu Mkuu wa EAC.

Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) limemripoti Bukuku kutoka katika mkutano wa kujadili mswaada wa maendeleo ya udhiti wa uzito wa magari ndani ya EAC, uliofanyika mjini Nairobi Juzi.

Alifafanua kwamba kuoanisha kwa sheria za udhibti wa uzito wa magari kutapunguza kwa kiasi kikubwa gharama hususan ni kwa nchi ambazo hazina njia za usafirishaji wa bahari kama vile Uganda, Rwanda na Burundi.

Mswaada huo ujulikanao kama Mswaada wa Udhibiti Uzito wa Magari wa EAC, 2012, ni hatimishao la majadiliano yaliyochukua mwaka mzima ambapo nchi wananchama zilijadilia kwa kina taarifa za kiufundi juu ya uzito wa magari.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Ushirikiano la Kimataifa la Japan (JICA) ulipendekeza kwamba kanda hiyo ikubaliane kuoanisha viwango vya uzito wa juu kabisa wa magari, kutoruhusu uzito wa kupita kiasi na kuwekwe vituo vya kupima uzito wa magari barabarani.

Hivi sasa nchi za kanda hii ya Afrika Mashariki zina viwango tofauti vya uzito wa magari unaoruhusiwa kwenye barabara zake ambao ipo haja za kuuoanisha. Nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi unaruhusu uzito wa juu wa tani 56 kwa lori moja, wakati Uganda inaruhusu tani 53 huku Kenya tani 48.

Katika majadiliano yaliyofanyika imekubalika kwamba kanda iwe na kiasi cha juu cha uzito wa magari unaoruhusiwa kuwa ni tani 56.

Kwa mujibu wa Bukuku, Sekretarieti ya EAC inatarajiwa kukamilisha mswaada huo na kuufikisha kwenye Bunge la Afrika Mashariki (EALA) ifikapo Aprili na hatimaye kupitishwa kuwa sheria ifikapo Juni, mwaka huu.