Shahidi kesi ya Lema ajichanganya

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA)

Na Mwandishi Wetu, Arusha

SHAHIDI wa tano wa kesi ya kupinga matokeo ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) ya mwaka 2010, Arafa Mohamed amejikanganya katika maelezo alioyatoa mahakamani jana.

Mbele ya Jaji Gabriel Rwakibarila anayesikiliza shauri hilo, shahidi huyo alipokuwa anaongozwa na Wakili wa upande wa walalamikaji, Modest Akida, shahidi huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa wakati wa kampeni alihudhuria mikutano ya kampeni za vyama vya CCM, CHADEMA, UDP na NCCR Mageuzi.

Awali alipokuwa akihojiwa na Wakili wa Mlalamikiwa wa kwanza (Lema) Method Kimomogoro shahidi huyo alidai mahakamani hapo kuwa hakuudhuria mikutano ya NCCR-Mageuzi na UDP.

Mahojiano kati ya shahidi na wakili Kimomogoro ilikuwa kama ifuatavyo: Wakili: Wakati unaongozwa na Wakili wa walalamikaji ulisema umehudhuria mikutano ya NCCR Mageuzi na UDP, hebu ieleze Mahakama ni katika maeneo gani na kata gani ulihudhuria mikutano ya vyama hivyo?

Shahidi: Nilikosea sikuhudhuria mikutano ya NCCR Mageuzi wala ya UDP, nilisahau kwa sababu ni muda mrefu umepita tangu uchaguzi ufanyike, nilihudhuria mikutano ya TLP na CUF.

Akiongozwa na wakili aliieleza mahakama kuwa wakati wa kampeni Kata ya Elerai Septemba 6, 2010 kwenye mkutano wa CHADEMA, wakati Lema anajinadi na kuomba kura aliwataka wananchi wasimchague Batilda aliyekuwa mgombea wa CCM.

“Alituambia wananchi wa Elerai naomba kura zenu kwa sababu huyo mgombea sasa ni mjamzito akijifungua hataweza kukaa jimboni kwa sababu si mkazi wa Arusha kwa wapiga kura wake,” alimnukuu Lema, shahidi huyo.

Alidai kuwa katika mkutano uliofanyika eneo la Mbauda Kata ya Sombetini Septemba 9, Lema aliwatahadharaisha wakazi wa jimbo la Arusha kutomchagua aliyekuwa mgombea kupitia CCM kwa madai kuwa ni mwanamke. “Aliwatahadharisha wananchi wa Jimbo la Arusha kwa kuwaeleza kuwa, Waarusha msije mkakubali kuongozwa na mwanamke,” alidai shahidi.

Awali Kimomogoro aliiomba mahakama kupinga ushahidi huo uliokuwa unatolewa na shahidi huyo kwa madai kuwa hakuna mlalamikaji hata mmoja ambaye ametoa ushahidi katika maeneo aliyoyasema Shahidi huyo.

“Mheshimiwa Jaji walalamikaji walisema kuwa hawamuwakilishi mtu yoyote na walidai kuwa hawakuhudhuria mikutano mingine zaidi ya ile waliyoitolea ushahidi na hayo mambo mengine yaliyofanyika katika mikutano mingine ni ya kusikia kwa sababu hiyo Mheshimiwa Jaji tunaomba ushahidi huu wa bi Arafa usipokelewe, kwani walalamikaji nao walikanusha mbele yako kuwa hawakuzungumza na mtu yoyote zaidi ya Dk. Batilda,” alisema Kimomogoro.

“Mheshimiwa Jaji shahidi wa nne alipotoa ushahidi wake hatukuuupinga, ila kam walalamikaji wangesema waliongea na watu wengine waliohudhuria mikutano mingine ya kampeni, tusingepinga kupokelewa kwa ushahidi wa shahidi huyu, walete mashahidi ambao watazungumzia yale walalamikaji waliyotolea ushahidi,” alisema

“Mahakama ni mahali ambapo mtu anakuja kuomba nafuu ya kisheria na waliokuja kuomba nafuu huyo hapa ni walalamikaji ambao waliieleza Mahakama kuwa waliathirika kidini, kijinsia na kikabila ila shahidi huyo sasa anataka kutumia mlango wa shahidi kuwa mlalamikaji, naona shahidi huyu ameletwa hapa kutalii, mahali hapa si pa kutalii ni pa kutafuta haki kwani hapa siyo mbuga za wanyama,” alisema wakili wa serikali Timon Vitalis.

Wakili wa walalamikaji, Akida alisema kuwa ntafsiri ya malalamiko ya mawakili wa utetezi, walichokuwa wanazungumza kiliashiria walalamikaji wasipeleke mashahidi mahakamani, kitu ambacho alidai hakiwezekani. Baada ya mabishano hayo ya kisheria Jaji Rwakibarila alikataa maombi hayo ya Kimomogoro na shahidi huyo aliendelea na ushahidi wake.

Alisema kwa mujibu wa kipengele cha 7 na 8 vinavyosimamia ukiukwaji wa sheria nchini ni yale ambayo yalitokea wakati wa tukio, na sababu zilizotolewa na mawakili wa pande zote, hazikidhi matakwa ya sheria.

Aidha shahidi huyo alipoulizwa amekuja mahakamani hapo kumtolea nani ushahidi, alisema kuwa aliitwa na Musa Mkanga (mlalamikaji wa kwanza) katika shauri hilo. Shahidi huyo alidai mahakamani hapo kuwa hakuridhika na matokeo ya uchaguzi huo kutokana na kauli aliyoitoa Lema kuwa Batilda siyo mkazi wa Arusha, jambo lililowafanya wapiga kura wasimchague.

“Sikuridhika na matokeo kwa sababu sisi wanawake tumedhalilika kuwa hatuwezi kuongoza nchi, nilimweleza Musa kutokana na sababu za mheshimiwa (Batilda) si mkazi wa Arusha hivyo asilimia 80 yaa watu hawakumchagua,” alidai mahakamani hapo.