Vodacom yashusha gharama za M-Pesa asilimia 75

Nembo ya Kampuni ya Vodacom

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya huduma za simu za mkononi inayoongoza nchini leo imetangaza kwa wateja wake ofa 4 kwa pamoja zitakazowafanya wazidi kufaidika, kuwezeshwa pamoja na kufurahia huduma za Vodacom M-Pesa.

Wateja wa M-Pesa sasa wamepunguziwa gharama za kufanya miamala kupitia huduma hiyo ambapo sasa kila muamala utagharimu sh. 50 ikiwa ni punguzo la asilimia 75. Wakati huo huo Vodacom imeongeza kiwango ambacho mteja anaweza kununua muda wa maongezi kupitia huduma hiyo ya M-Pesa hadi asilimia 25 kutoka asilimia 10 ya sasa.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Rene Meza amesema; “Tunatambua ni kwa kiwango gani huduma ya M-Pesa imekuwa ya umuhimu kwa maisha ya kila siku ya Watanzania, hivyo ni jambo la muhimu pia kwetu kuwapatia ofa zinazoakisi matumizi yao na kuyafanya kuwa rahisi na nafuu zaidi. Hii ndio dira yetu kwa mwaka huu na kuendelea,” Alisema Meza.

Ofa nyengine iliyotangazwa na kampuni ya Vodacom Tanzania ni inayomwezesha mteja wa M-Pesa sasa kuweza kutuma kiasi cha chini zaidi cha fedha cha sh. 500 kupitia simu yake ya mkononi. Meza ameielezea ofa hii kuwa inalenga kuhakikisha kila Mtanzania bila kujali hali yake ya kiuchumi anafaidika na huduma bora, salama, ya uhakika na kuaminika ya M-Pesa.

Aidha, pamoja na ofa hizo, kampuni ya Vodacom imezindua pia promotion ya M-Pesa ambapo jumla ya sh. 480 milioni zitashindaniwa na wateja kadri ambavyo wanavyotumia huduma ya M-Pesa.

Katika promosheni hii wateja 100 watakuwa wakijishindia zawadi ya fedha taslimu za kitita cha sh. 50,000 kwa kila mshindi kupitia droo zitakazochezeshwa kila siku huku droo kuu ya kila mwezi kwa miezi mitatu ikitoa mshindi wa sh. 10 milioni. Promosheni hiyo itadumu kwa siku tisini kuanzia Februari 13, mwaka huu.

“Dhamira yetu ni ya dhati kuhakikisha wateja wetu wanakuwa na furaha wakati wote na huku tukiwawezesha kadri wanayotumia huduma ya MPESA. Tutaendelea kuboresha mfumo wa M-Pesa sambamba na huduma zinazopatikana katika MPESA ili izidi kuendana na mahitaji halisi ya maisha ya kila siku ya wateja.” Alisema Meza.

Kupitia huduma ya M-Pesa mteja anaweza kufanya malipo kwa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo kununua umeme – LUKU, kulipia DAWASCO na DSTV. Aidha huduma ya m-pesa inaweza pia kutumika kulipia tiketi za usafiri wa ndani wa anga kwa mashirika ya ndege ikiwemo Precision Air na Coastal Air, kulipia ada za shule, kuweka na kutoa fedha katika akaunti ya Benki ya CRDB na huduma nyengine nyingi.

Hakuna shaka huduma ya Vodacom M-Pesa ndiyo huduma ya kibenki kupitia simu za mkononi inayoongoza nchini ikiwa na mtandao mpana wa mawakala zaidi ya 18,000 walionena nchi nzima mijini na vijijini na inayokua kwa kasi. Ubora na umashauri wa huduma hii unaifanya kampuni ya Vodacom kuzidi kung’ara na kuongoza soko la huduma za simu za mkononi nchini.