Taarifa ya utafiti juu ya hali ya Shule za Sekondari za Kata Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa
Mwandishi: Joachim Mushi
Gazeti: Jambo Leo
Anwani: S. L. P 18180, Dar es Salaam
Simu: 0717 030 066, 0755 701 199
Barua: jomushi79@yahoo.com au dev.kisakuzi.com
March, 2011
Taarifa fupi ya eneo lililofanyiwa utafiti
Wilaya ya Nkansi ni moja kati ya wilaya za Mkoa wa Rukwa. Katika sensa ya mwisho yaani iliyofanyika mwaka 2002, Wialaya ya Nkasi ilikuwa na wakazi 208,497. Hata hivyo idadi hiyo itakuwa imeongezeka kiasi kikubwa kutokana na kukua kwa mji huo tangu ifanyike sensa ya mwisho (2002).
Idadi kubwa ya wakazi wa Wilaya ya Nkasi ni wafipa, wananchi ambao ndio wazawa wa eneo hilo kihistoria. Shughuli kubwa ya wakazi wa eneo hilo hasa wazawa ni wavuvi japokuwa wapo wengine ni wakulima pia.
Utafiti umeendeshwa kwa njia anuai kulingana na mazingira husika, ili kupata taarifa kadri zilivyokuwa na umuhimu katika shughuli nzima. Utafiti umefanyika kwa mahojiano ya mtu mmoja mmoja, makundi muhimu kwenye utafiti kulingana na uhitaji wa taarifa husika.
Miongoni mwa makundi hayo ni walimu wakuu, walimu wa kawaida, wananchi, viongozi wa manispaa, Serikali (wilaya), wazazi/walezi na baadhi ya wanafunzi. Wengine ni pamoja na viongozi wa asasi wadau wa elimu na wadau wengine muhimukatika sekta ya elimu kwa jumla.
Taarifa Kamili ya Utafiti
Wilaya ya Nkasi yaweza kuwa moja ya maeneo yaliyonufaika na ujenzi wa shule za kata kwa kiasi kikubwa. Nasema hivyo maana kabla ya kuanza kwa ujenzi wa shule hizo wilaya ilikuwa na shule moja tu ya sekondari yaani Nkasi Sekondari.
Ujenzi wa shule za sekondari za kata umeongeza idadi kubwa ya sekondari na sasa wilaya hiyo imefikisha sekondari 21, yaani shule 20 zote zikiwa zimejengwa baada ya kuanza kwa utaratibu wa shule za kata.
Utafiti umefanyika katika shule nne za kata ambazo mbili zinatoka katikati ya Mji wa Namanyere, ambao ni makao makuu ya Wilaya ya Nkasi na zingine mbili zinatoka nje kabisa ya mji huo ili kupata utofauti ya kimazingira.
Ni wazi kuwa Wilaya ya Nkasi imefanya vibaya kwenye matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka uliopita (2010), ambayo kiasi kikubwa yametokana na shule za sekondari za kata. Takwimu zinaonesha kati ya wanafunzi 659 waliotahiniwa mtihani wa Taifa kidato cha nne katika wilaya hiyo ni wanafunzi 39 pekee ndio waliofaulu.
Watahiniwa 620 wote walifeli. Matokeo halisi yalikuwa kama ifuatavyo;- hakukuwa na mwanafunzi yeyote aliyepata daraja la kwanza, waliopata daraja la pili walikuwa ni tisa (9), waliopata daraja la tatu walikuwa ni thelathini (30), waliopata daraja la nne ni mia tatu (300), huku waliopata daraja ziro (0) wakiwa mia tatu na ishirini (320).
Matokeo haya ni kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Nkasi, baada ya mahojiano na Katibu na Mwenyekiti wa chama hicho. Taarifa hizi za kufanya vibaya kwa matokeo hayo pia zilitolewa na ofisi ya halmashauri (elimu ya sekondari) na baadhi ya shule.
Utafiti unaonesha kufanya vibaya kwa wanafunzi wa shule hizi kumechangiwa na sababu nyingi. Miongoni mwa sababu kubwa ni ukosefu wa walimu wa masomo mbalimbali hasa ya Sayansi na Kiingereza, ukosefu wa walimu wenye sifa, ukosefu wa zana na vifaa vya kufundishia, mwamko mdogo wa elimu kwa wazazi na wanafunzi na uduni wa hali ya maisha kwa familia nyingi.
Kimsingi ni kweli baada ya kutembelea baadhi ya shule na kufanya mahojiano na vyanzo na wadau wa elimu mbalimbali wamethibitisha kuna upungufu wa walimu katika shule za kata eneo hilo lakini si kwa kiasi cha kutisha. Wastani wa idadi ya wanafunzi na walimu kwa shule si mbaya. Shule nyingi zipo ndani ya wastani wa taifa yaani mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40 (1:40).
Mfano kwa shule nne zilizofanyiwa utafiti, yaani shule za sekondari Mkangale na Nkomolo zilizopo katikati ya mji na shule za sekondari Mashete na Mkole za nje ya mji. Sekondari ya Mkangale ina jumla ya wanafunzi 279 ambao ni kidato cha kwanza hadi cha tatu. Shule hii ina walimu watano (5), hivyo wastani mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 55 (1:55).
Nkomolo ina wanafunzi 221 ambayo ina kidato cha kwanza hadi cha tatu, idadi ya walimu ni saba (7). Hivyo wastani wa mwalimu mmoja ni wanafunzi takriban 32, yaani (1:32). Kwa shule ya Sekondari Mashete wastani ni 1:23, huku Shule ya Sekondari Mkole wastani wa mwalimu mmoja ni wanafunzi 38 yaani 1: 38.
Ukiangalia kwa makini utaona kati ya shule nne zilizotembelewa ni moja tu ndio imezidi wastani wa taifa kiufundishaji na idadi ya walimu yaani shule ya sekondari Mkangale. Shule zote nne zililalamika hazina walimu wa masomo ya sayansi na lugha (Kiingereza), yaani Kemia, Fizikia, Biolojia, Hisabati pamoja na Kiingereza.
Hata hivyo zipo ambazo zimeonekana ama zina mwalimu mmoja au wawili ambao hawakidhi mahitaji ukilinganisha na idadi ya madarasa. Zipo ambazo zimeonekana hazina kabisa walimu wa baadhi ya masomo kama Kiingereza, Fizikia, Biolojia na Hesabu.
Shule ya Sekondari Mashete haina kabisa walimu wa masomo ya Fizikia, Kemia, Biolojia na Hisabati. Shule ya Sekondari Mkole haina kabisa mwalimu wa Kiingereza madarasa yote. Shule ya Sekondari Nkomolo haina kabisa mwalimu wa Fizikia.
Sekondari ya Mkangale haina kabisa mwalimu wa somo la Biolojia, japokuwa kwa masomo ya Kemia na Fizikia amekodishwa mwanafunzi wa kidato cha sita aliyehitimu mwaka jana ndiye anayeyafundisha masomo hayo mawili.
Zipo baadhi ya shule zimeamua kufuta kabisa masomo ya sayansi na kubaki zikifundisha masomo ya sanaa, kutokana na kutokuwa na walimu wa masomo hayo. Taarifa hii ni kwa mujibu wa Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Nkasi. Hata hivyo hakuna utaratibu kitaifa ambao unaruhusu shule kuondoa baadhi ya masomo kuanzia kidato cha kwanza.
Hali hii ya ukosefu wa walimu wa kutosha na wa baadhi ya masomo unaathiri kiasi kikubwa matokeo kiujumla. Mfano matokeo ya kidato cha pili kwa mwaka jana shule ya Mkangale inaonesha hakuna mwanafunzi aliyepata alama ya ‘A’ wala ‘B’, wanafunzi 16 tu ndiyo waliopata alama ‘C’, wanafunzi 41 waliambulia alama D na wanafunzi 53 walipata alama ‘F’. Kwa ujumla shule hiyo ilipata wastani wa ‘D’ ya 32 kiufaulu.
Katika baadhi ya shule wapo walimu ambao wanalazimika kufundisha masomo ambayo hawakuyasomea wakiwa chuoni kukidhi uhaba wa walimu wa masomo. Walimu hao wanafundisha masomo hayo kimazoea bila kozi yoyote. Waliohojiwa walikiri wanafundisha uzoefu wa madarasa waliopita kipindi wakiwa madarasa hayo kimasomo.
Katika Shule ya Sekondari Mkole walimu wawili wanafundisha masomo ambayo hawakupata mafunzo yake vyuoni, lakini wamelazimika kutokana na mazingira magumu ya uhaba wa walimu husika wa masomo. Kwenye shule hiyo yupo aliyesomea Biolojia na Kilimo, lakini amelazimika kufundisha Kemia; pia yupo aliyesomea Jiografia na Kiswahili lakini amepewa kufundisha somo la Uraia (Civics).
Kwa mujibu wa sera ya elimu na mafunzo (1995) inafafanua kuwa mwalimu wa sekondari anakuwa na sifa hiyo baada ya kuwa na diploma na shahada ya taaluma hiyo. Hata hivyo imefafanua zaidi mwalimu wa diploma anapaswa kufundisha kidato cha kwanza na cha pili. Huku yule wa shahada ya mafunzo ya ualimu akiruhusiwa kufundisha kidato cha tatu hadi cha nne.
Hali hiyo ni tofauti na utafiti eneo la Nkasi. Kati ya walimu 171 wa sekondari wenye shahada ni 24 pekee, walimu nane ni wa mfumo wa chap chap yaani wa kidato cha sita (walimu wa vodafasta) na waliosalia 139 ni walimu wa diploma.
Kwa mantiki hiyo ni walimu wachache sana wilayani Nkasi ndio wanasifa za kufundisha sekondari kidato cha tatu hadi cha nne. Hata hivyo hili aliangaliwi wala kuzingatiwa ipasavyo.
Shule nyingi zimeanza kazi bila vifaa na nyenzo muhimu za kufundishia na kujifunzia. Kati ya shule zote nne hakuna shule yenye maktaba, maabara wala stoo kwa ajili ya vifaa muhimu vya shule. Zote pia hazina ofisi za walimu na badala yake zimechukua moja ya darasa na kuligeuza ofisi ama stoo. Karibu zote hazina bodi ya shule licha ya kuwepo zingine kuendeshwa kwa zaidi ya miaka minne.
Nyingi hazina hosteli licha ya kuchukua wanafunzi kutoka vijiji vya mbali, ambao ulazimika kupanga vyumba jirani na shule jambo ambalo limefanya wengine kuingia na vishawishi. Idadi ya wanafunzi katika madarasa wamekuwa wakipungua toka kuchaguliwa baada yaw engine familia zao kushindwa kugharamia pango kutokana na ugumu wa maisha.
Watu waliohojiwa katika utafiti
1. Mwanaisha Luaga (Ofisa Tawala Wilaya ya Nkasi)
2. Abel Ntupwa – 0754858883 (Ofisa Elimu Sekondari)
3. Rodger Rutimba 0765335498 (Kaimu Mkuu wa Sekondari Nkomolo)
4. John Mpemba – 0786438420 (Mwalimu Mkuu Mkole Sekondari)
5. Elizaeli Komba – Mwalimu Sekondari ya Mkole
6. Rashid Kimata- Mwalimu Sekondari ya Mkole
7. Oswald Tambala – 0767014645 (Mwenyekiti CWT Wilaya ya Nkasi)
8. Bwana Nzunda – 0766836240 (Katibu CWT Wilaya ya Nkasi)
9. Raban Kapandila – 0752325320 (Kaimu Mkuu wa Sekondari Mashete)
10. Marry Kayombo- Mwalimu Sekondari ya Mashete.
11. Mwajuma Mboha – Mwalimu Sekondari ya Mashete.
12. Michael Kamfumu- Mwalimu Sekondari ya Mashete.
13. Awadhi Yusuf – 0766328261 (Kaimu Mkuu wa Sekondari Mkangale)
14. Leah Simpamba – Mwalimu Mkangale Sekondari.
15. John Simkonda – Mwalimu Mkangale Sekondari.
16. Wilson Mwampamba – Mwalimu Mkangale Sekondari.
17. Hussein Abdulah – Mwalimu Nkomolo Sekondari.
18. Rehema Samuel – Mwalimu Nkomolo Sekondari.
19. Oscar Msemwakweli – Mkazi ya Isunta Namanyere
20. John Samya – 0754960797- Mzazi
21. Frank Kipanga – Mzazi na mkazi wa Kilando.
22. Ester Mshiha – 0786443215 Mkazi – Nkasi
23. Teddy Mandona – Mzazi Nkasi
24. Edson Kaungula – Mwanafunzi
25. Zakayo Chilaya – mwanafunzi
26. Ashura Said – Mwanafunzi
27. Emmanuel Ewald – Mwanafunzi
28. Marry Frank – Mzazi Nkasi
29. Idd Ibrahim – Mwanafunzi
30. Gratian Mukoba- Rais wa CWT- Tanzania.
Taarifa ambazo hazikuripotiwa
Zipo baadhi ya taarifa ambazo hazikuripotiwa katika mfululizo wa habari na makala zilizotoka baada ya utafiti huu. Taarifa hizi nyingi ni zile zilizokuwa nje ya mwongozo wa dodoso za utafiti, japokuwa katika namna moja nazo zinaingiliana na suala zima lililofanyiwa utafiti.
Kwanza ni malipo ya stahili mbalimbali za walimu katika baadhi ya shule. Kati ya shule kadhaa zilizotembelewa na utafiti zimeonekana kuwa na malalamiko kwa baadhi ya malipo ambayo walimu wanaidai ama Serikali Kuu na mengine halmashauri ambazo kwa sasa ndio waajiri wa walimu.
Walimu wanaohamishwa ama kupangiwa sehemu za kazi (ajira) mpya hawalipwi kiasi chote cha fedha ambazo ni stahili mbalimbali. Kwa walimu wapo ambao bado wanadai sehemu ya malipo yao baada ya kulipwa nusu. Baadhi wamekata tamaa kama huenda baadaye wakalipwa kiasi wanachodai, kutokana na kuzunguzwa.
Kwa walimu wa muda mrefu wapo ambao ama wanadai stahili za uhamisho na stahili nyingine, jambo ambalo wengi hawaamini kama baadae watalipwa stahili hizo kutokana na danadana zinazofanywa kila wanapofuatilia.
Mwenyekiti wa CWT, Bw. Talamba akifanya mahojiano na utafiti huu alisema; “Wajua unapomzungumzia mwalimu kwa Wilaya ya Nkasi anachangamoto nyingi sana jambo ambalo wengi zinawakatisha tamaa, walimu wengi bado hadi leo wanadai stahili mbalimbali kama malipo ya uhamisho, fedha za likizo na stahili anuai…mtu kama huyu hawezi kufanya kazi kwa moyo wote na upendo.”
Kutokana na miundombinu duni ya barabara kuanzia maeneo ya mjini hadi inayounganisha maeneo mbalimbali ya vijijini, familia nyingi wakiwemo walimu wana hali mbaya kimaisha jambo ambalo linachangia kwa namna moja ama nyingine. Yapo maeneo ambayo magari huenda kwa msimu jambo ambalo huchangia hata huduma za jamii kuwa ghali na duni.
Barabara si za uhakika na mvua zinapoanza hali ya usafiri huwa mbaya zaidi kwa maeneo ya vijijini ambayo mengi ni pembezoni mwa Ziwa Rukwa na Tanganyika ambako wananchi wengi hutegemea shughuli za uvuvi.
Pamoja na hayo hakuna usafiri wa uhakika kwa maeneo mengi hasa vijiji kama vile kutoka Mwampembe kuja mjini. Maeneo haya yana shule na walimu ambao hulazimika kutembea umbali mrefu kwenda vijiji vya jirani na kuvizia magari kwa ajili ya kwenda mjini, ikiwemo kufuatilia mishahara yao na mahitaji mengine.
Watumishi kama walimu hulazimika kutumia sehemu kubwa ya mishahara yao kufuatilia mishahara kila mwezi jambo ambalo huathiri pia masomo, mwalimu aweza kutumia zaidi ya wiki moja kufuatilia mishahara hiyo kutokana na ugumu wa usafiri.
Suala lingine ni kuwepo imani za kishirikina ambapo limekuwa likiwatisha walimu hasa wale wanaokuja kutoka mikoa mingine. Wapo baadhi ya wanafunzi na watumishi wa sekta mbalimbali ambao walionekana kulitaja suala hilo na kudai linaathiri elimu kutokana na vitendo vya kishirikina kujitokeza baadhi ya shule.
Hitimisho kwa kifupi
Kimsingi sehemu kubwa ya mambo ambayo nilikwenda kutaka kujua kiundani, imebainika yanafanywa ndivyo sivyo kwa shule chache tu nilizofanikiwa kuzitembelea. Niweke wazi kuwa ujenzi wa shule za kata unatekelezwa kisiasa zaidi bila kujali umuhimu wa sekta yenyewe (ya elimu).
Shule za kata zinaanzishwa bila kuwa na nyenzo zote muhimu hivyo kuendeshwa mithili ya sehemu ya majaribio ya mfano wa shule. Zipo shule zimeanzishwa na kupokea wanafunzi ikiwa na mwalimu mmoja tu ili hali kuna zaidi ya masomo tisa ambayo yanapashwa kufundishwa.
Shule inaanzishwa haina walimu wala vitabu vya kufundishia. Shule inaendeshwa zaidi ya miaka mitatu bila kuwa na ofisi, maktaba, maabara na hata stoo za shule kwa ajili ya kuhifadhia nyenzo muhimu za shule. Shule hazi waalimu wa masomo ya sayansi kama Kemia, Biolojia, Fizikia, Hisabati na pamoja masomo ya lugha yaani Kiingereza.
Pia shule hazina walimu wa kutosha na wenye sifa za kufundisha hivyo walimu wakuu kulazimika kuchukua wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na sita kurudi katika shule hizo kwa lengo la kuwafundisha wanafunzi masomo ambayo yamekosa walimu kwenye shule hizo.
Zipo shule ambazo zimelazimika kufuta masomo ya sayansi na kuanza kufundisha yale ya sanaa pekee ili kujitahidi kufuta hali ngumu za upungufu mkubwa wa walimu unazozikabili shule. Lakini kama hiyo haitoshi shule nyingi za kata zinaanzishwa pasipo kuzingatia mwelekezo wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, ambayo inatoa maelekezo mwalimu ni mtu gani na kutaja kazi na ngazi anazopaswa kufundisha.
Kifupi mwalimu wa ngazi ya diploma anapaswa kufundisha kidato cha kwanza na cha pili, walimu mwenye ngazi ya shahada wanapaswa kufundisha kidato cha tatu na cha nne na si vinginevyo.
Hata hivyo idadi kubwa ya walimu waliopo shule nyingi za kata ni wa ngazi ya diploma ambao wanafundisha madarasa yote bila kuzingatia Sera Elimu na Mafunzo. Kimsingi hali hii ni kinyume na utaratibu ambao sekta ya elimu imejiwekea katika kulingana na umuhimu suala zima la elimu, naamini hili laweza kuchangia elimu yetu kuendelea kufanya vibaya katika ngazi mbalimbali nchini ikiwemo ya sekondari.
Mapendekezo
Kimsingi ujenzi wa shule za serikali za sekondari ni jambo la msingi kwa kuwa linasogeza huduma hiyo kwa jamii husika. Ni vema basi ufanyike utafiti kabla ya ujenzi wa shule hizi, kwamba eneo husika lina miundombinu ya kutosha ambayo haiwezi kuwa kikwazo kwa uendeshaji shughuli za shule kwa wanajamii.
Kabla ya kuanzishwa kwa shule kuna kila sababu vyombo husika kujua kitapata wapi mahitaji yote ya shule; kama walimu wa kutosha, majengo muhimu yakiwemo madarasa, ofisi za walimu, maktaba, stoo pamoja, nyumba kadhaa za walimu pamoja na nyenzo stahili za shule. Hii ni kutokana na sasa jamii kujengewa hata madarasa mawili ama matatu eneo fulani bila kifaa chochote nao kukubali hiyo ni shule na kuanza kupokea wanafunzi.
Serikali iisamini elimu ya sekondari kutokana na umuhimu wake, kwani tunapoelekea elimu hii yaweza kuwa haina maana yoyote. Kama imeonekana shule kama ya sekondari yaweza kuanzishwa eneo fulani bila kuwa na vifaa vyovyote muhimu hii ni hatari.
Serikali iache kuridhia wanafunzi wa kidato cha nne kuwa walimu katika shule za kata kuendeleza tabia hii ni kuwajaza ujinga wanafunzi wa shule za kata nao kudhani wanajua kumbe hakuna wanachokijua, kwani si kila mtu anaweza kuwa mwalimu mzuri wa kufundisha mwanafunzi.
Kuna kila sababu ya Serikali kuthamini taaluma ya ualimu kwa kuwajali na kuwathamini walimu katika ngazi mbalimbali hali hii itasaidia kuwajengea heshima nao kufanya kazi kiufasaha na kupata mazao bora. Walimu wataguswa na matokeo mabaya ya wanafunzi wanaowafundisha kama nao watajaliwa kwa kila hali kama watumishi wengine mihimu.
Ni bora tuwe na shule chache lakini zinatoa wanafunzi waliofunzwa na kuelimika kweli kweli, kuliko kuwa na shule nyingi lakini zinatoa elimu ya kubabaisha-yaani tunakuwa na lundo la watu waliopata elimu ya sekondari lakini hawawezi kutofautishwa na wale wa shule za msingi kutokana na uelewa sawa.
Mwisho