Kozi ya makocha angazi pevu yaahirishwa

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeahirisha kozi ya ukocha ngazi pevu (Advanced Level) iliyokuwa ifanyike jijini Dar es Salaam kuanzia Februari 12- 25 mwaka huu.

Kozi hiyo imeahirishwa kwa vile wengi wa makocha walioomba hawakufikia vigezo vilivyowekwa. Vigezo vya msingi vilikuwa mwombaji awe na cheti cha ukocha ngazi ya kati (Intermediate Level), wawe wanafanya kazi hiyo ya ukocha (active) na kuwasilisha cheti cha elimu ya sekondari (kidato cha nne).

Mwisho wa kuwasilisha maombi kwa ajili ya kozi hiyo ilikuwa Februari 5 mwaka huu. Makocha 34 waliwasilisha maombi kwa ajili ya kushiriki kozi hiyo, lakini waliokidhi vigezo ni 12 tu.

Makocha waliokidhi vigezo kwa ajili ya kozi hiyo ni Sospeter Vedasto kutoka mkoani Pwani, Beatus Manga (Temeke), Renatus Shija (Pwani), Ntungwe Selemani (Pwani), William Mamiro (Kinondoni), Ngawina Ramadhan (Temeke), Khatib Mtoo (Temeke), Hamisi Chimgege (Temeke), Selemani Mkumya (Temeke), Idd Cheche (Azam), Mohamed Mayosa (Temeke) na Imam Mbarouk (Shinyanga).

Wawezeshaji wa kozi hiyo ambayo sasa tarehe yake ya kufanyika itatangazwa baadaye ni Mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Jan Poulsen, Mkufunzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni na Mkufunzi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU), Kim Poulsen.

Wakati huo huo; mshambuliaji Kipre Bolou Wilfried aliyejiunga na Azam kutoka Ivory Coast sasa ni ruksa kuichezea timu hiyo michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali nchini.

Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ivory Coast (FIF) jana (Februari 9 mwaka huu) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji huyo aliyeombewa uhamisho katika dirisha dogo la usajili kutoka timu ya Sewe Sport ya nchini humo.