JK akutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bw. Johhnie Carlson na Ujumbe wake pamoja na waziri wa Nishati na Madini, Williuam Ngeleja walipomtembelea Ikulu jijini Dar es Salaam leo January 9, 2012

Na Mwandishi Maalumu

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete, leo katika Ikulu ya Dar es Salaam, amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Johnie Carsons.
Katika mazungumzo yao, Rais Kikwete amemwambia, Carsons kuwa Serikali inakaribisha wawekezaji kutoka Marekani kwenye sekta mbalimbali hasa sekta ya nishati ambayo inahitajika sana kwani lengo la Serikali ni kupata megawati elfu tatu (3000) ifikapo mwaka 2020.
“Tunahitaji uwekezaji katika kufikia malengo yetu ya umeme utakaotosheleza mahitaji yetu, Serikali haiwezi kufanya uwekezaji huu pekee yake, tunahitaji wawekezaji binafsi,” rais amesema na kuishukuru Marekani kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, afya, nishati na nyinginezo.
Carsons yuko katika ziara ya kutembelea Afrika na amewasili nchini jana akitokea Msumbiji. Nchi zingine anazotarajiwa kutembelea akitokea Tanzania ni Nigeria na Ghana.
Mbali na maafisa wa Serikali ya Marekani, Carsons ameambatana na wafanyabiasahara wa Marekani walioko katika sekta ya nishati, ambao wanatarajiwa kufanya mazungumzo na Serikali katika nia ya kuwekeza zaidi. Kampuni hizo ni Anadarko Petroleum Corporation, Caterpillar, Chevron, Energy International na General Electric.
Wengine ni Pike Electric Corporation, Strategic Urban Development Alliance (SUDA), Symbion and Zanbato ambayo inashughulika na kutoa nafasi za uwekezaji na masoko kupitia njia ya mtandao ujumbe huo pia umejumuisha mashirika ya serikali kama Corporate Council on Africa (CCA) na Wakala wa Biashara na Maendeleo wa Marekani ( USTDA).
Tayari kampuni ya Symbion imewekeza hapa nchini katika sekta ya Nishati ambapo hadi sasa imeishawekeza megawati 50 mkoani Arusha, Mw 112 Dar es Salaam, na Mw 50 mjini Dodoma. Symbion pia imeanza kuwekeza jumla ya Mw 50 mjini Morogoro na zingine 50 mjini Mwanza.
Katika shughuli nyingine, leo Rais Kikwete ameagana na Balozi Liu Xinsheng wa China ambaye amemaliza muda wake hapa nchini. Rais Kikwete ameishukuru China kwa mchango wake mkubwa kwa Tanzania na kuelezea kuwa China imeshirikiana vyema na Tanzania katika masuala mbalimbali ya kitaifa na Kimataifa