Na Janeth Mushi, Arusha
UPANDE wa wadai katika kesi ya kupinga matokeo ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) unatarajia kuanza kutoa ushahidi wake leo katika mahakama kuu Kanda ya Arusha. Wakili wa upande wa wadai Alute Mughwai, alisema kuwa wanatarajia kuwa na mashahidi zaidi ya 25, ambapo leo mashahidi wawili anatarajiwa kutoa ushahidi wao.
Aidha kesi hiyo ambayo ilikuwa ianze kusikilizwa leo mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Sumbawanga, Gabriel Rwakibarila, haikuweza kufanyika baada ya Mawakili wa pande zote mbili kufanya vikao vya mara kwa mara na Jaji, kwa lengo la kukubaliana na taratibu zitakazowawezesha kuendelea na shauri hilo.
Hali hiyo ilijotokeza leo mahakamani hapo, kutokana na Jaji Rwakabarila kuteuliwa kusikiliza kesi hiyo baada ya kujitoa Jaji Aloyce Mujulizi aliyekuwa akiisikiliza awali.
Jana kesi hiyo ilitarajiwa kuanza majira ya asubuhi, lakini kutokana na vikao hivyo baina ya Mawakili na Jaji, kesi hiyo haikuweza kusikilizwa licha ya wananchi kuwepo ndani ya ukumbi wa mahakama hadi majira ya 2:45 walipopewa taarifa kuwa kesi hiyo imeahirishwa hadi leo.
Lema anatetewa na wakili Method Kimomogolo kama mshitakiwa wa kwanza na mshitakiwa wa pili Mwanasheria wa Mkuu wa Serikali akitetewa na Juma Masanja.
Kesi hiyo namba 13/2010 imefunguliwa na wapiga kura watatu katika Jimbo la Arusha Mjini ambao ni Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo ambao kwa pamoja wanaiomba mahakama hiyo kutengua ushindi wa Lema kwa madai ya kukiuka sheria wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.