Mgomo wa madaktari; Wanaharakati, wananchi wafunga barabara kwa maandamano Dar

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba akizungumza na waandishi wa habari eneo la Daraja la Salenda jijini Dar es Salaam, kutoa ufafanuzi juu ya maadamano ya wanaharakati pamoja na baadhi ya wananchi yaliofanyika kuishinikiza Serikali kuchukua hatua na kutatua mgomo wa madaktari unaoendelea maeneo mbalimbali nchini.

Baadhi ya magari ya msafara wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda yakipita eneo ambalo wanaharakati walikuwa wamezuia barabara magari kupita eneo la Palm Beach.

*Ni ile muhimu inayotumiwa na vigogo Dar, lengo ni kuitaka Serikali izungumze

Na Joachim Mushi

WANAHARAKATI pamoja na wananchi kadhaa jijini Dar es Salaam leo wameandamana na kuziba moja ya barabara muhimu ambayo hutumiwa na viongozi wakuu wa nchi akiwemo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye nusura msafara wake uzuiwe akitokea nyumbani kwake.

Barabara iliyofungwa kwa muda ni ile ya Ali Hassan Mwinyi katika makutano ya taa za kuongozea magari na ile ya Ocean Road jirani na Kituo cha Daladala cha ‘Palm Beach’ hatua chache kutoka Daraja la Salenda, barabara hii hutumiwa zaidi na viongozi wa juu serikalini.

Waandamanaji hao ambao walikuwa na mabango yaliyokuwa na jumbe mbalimbali za kuishinikiza Serikali kuridhia madai ya madaktari waliopo katika mgomo takribani wiki ya tatu sasa, waliziba barabara kwa takribani nusu saa hali ambayo ilileta msongamano mkubwa wa magari.

Hata hivyo nusura kadhia hiyo iukumbe msafara wa Waziri Mkuu Pinda ambaye alikuwa akitokea nyumbani kwake kuelekea mjini. Wakizungumza na wanahabari baadhi ya wanaharakati walisema walifikia hatua hiyo ili kufikisha kilio chao cha kuwatetea Watanzania wagonjwa ambao wamekuwa wakifa huku wengine wakitaabika wiki ya tatu sasa mgomo wa madaktari ukiendelea nchi nzima.

Miongoni mwa wanaharakati hao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Ananilea Nkya ambaye alisikika akipaza sauti kuwa kuna haja ya Serikali na Bunge kulichukulia suala la mgomo wa madaktari kwa udharura, kwani hali ni mbaya katika hospitali mbalimbali ikiwemo ile ya taifa Muhimbili.

Huko Dodoma bungeni suala hilo limeendelea kuwakera baadhi ya wabunge na kuliomba Bunge liache shughuli zake za sasa na kujadili mgomo wa madaktari. Aliyechokoza hoja hiyo bungeni leo akiwa mbunge wa sita kwa mara tofauti ni Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Selukamba, alimuomba Naibu Spika Job Ndugai aliyekuwa akiongoza bunge kuliona suala hilo la dharura na iruhusiwe bunge lianze kujadili.

Baada ya hoja hiyo Naibu Spika wa Bunge, Ndugai alisimama na kutoa ufafanuzi kuwa umefika wakati kuliangalia tena. “Utendaji mzuri wa bunge wa utoaji uamuzi ni pamoja na kupata ushauri kutoka kwa Kamati ya Uongozi ya Bunge…hivyo nawaomba wajumbe wa kamati hii tukutane katika Ukumbi wa Spika baada ya shughuli hizi ili tujadiliane kwa pamoja,” alisema Naibu Spika.

Alieleza kuwa hoja hiyo imewasilishwa bungeni na wabunge tofauti kwa mara sita sasa hivyo ni vigumu kwa meza yake kuendelea kunyamaza juu ya suala hilo.

Hata hivyo, Ndugai aliendelea kutoa ombi kwa madaktari kote nchini kurudi kazini na kuachana na mgomo unaoendelea huku ikiitaka Serikali iendeleze juhudi za kusikiliza jambo hilo kwa usalama na amani ili kuokoa maisha ya watu wanaoteseka kutokana na mgomo.

Baada ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kusitisha huduma zake tangu jana hali imeendelea kuwa tete kwa hospitali binafsi sasa kwani zimefurika wagonjwa kiasi cha kushindwa kutoa huduma kama zilivyokuwa zikitoa awali.

Akizungumza leo na vyombo vya habari Mkurugenzi wa Hospitali ya Mission ya Kairuki Dk. Asser Mchomvu amesema kwa sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa katika hospitali hiyo tofauti na ilivyokuwa awali jambo ambalo linawaelemea kutokana na nguvu kazi ndogo.

Amesema awali kwa siku hospitali hiyo hupokea wagonjwa 300 hadi 400, lakini kuanzia jana wamekuwa wakipokea wagonjwa 600 hadi 700 jambo linalofanya huduma inayotolewa kutokuwa ya haraka kama ilivyokuwa mwanzo.

Dk. Mchomvu amesema ongezeko hilo limesababisha fujo nyingi kwani kila mmoja anataka mgonjwa wake ahudumiwe kwa wakati kutokana na hali ya wagonjwa hao kuwa mbaya. Mmoja wa wagonjwa Lusi Shayo amesema wameamua kwenda katika hospitali binafsi ili kunusuru afya zao baada ya hospitali ya taifa Muhimbili kufungwa.

Taarifa ambazo mtandao huu umezipata leo na Hospitali ya Rufaa ya Bugando Mwanza nayo imesimamisha huduma zao zote hata zile za dharura baada ya madaktari wengi kuanza mgomo wakiungana na wenzao mikoa tofauti.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini (TAMWA), Ananilea Nkya akiwa ameshikilia moja ya bango lililokuwa na ujumbe wa maandamano hayo wakati wa maandamano Dar es Salaam hata hivyo maandamano hayo yalitawanyika muda mfupi baada ya askari polisi kufika.