Tume ya Uchaguzi Tanzania yaanza kumtafuta mrithi wa marehemu Sumari

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji msataafu Damian Lubuva

Na Mwandishi Wetu

TUME ya Taifa ya Uchaguzi imepanga kufanya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Jeremiah Solomon kufariki dunia hivi karibuni.

Taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na Mweneyekiti wa Tume hiyo, Damian Lubuva imesema ratiba ya kufanyika kwa Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki itaanza kwa uteuzi wa wagombea machi 08, mwaka huu, ambapo kampeni za uchaguzi zitaanza machi 09 hadi 31 na siku ya upigaji kura itakuwa Aprili Mosi mwaka huu.
Aidha, Tume hiyo imesema kuwa itafanya Chaguzi Ndogo za Madiwani katika Kata nane (8) zilizoko katika Halmashauri mbalimbali nchini kufuatia kuwepo wazi kwa nafasi za Viti vya Madiwani ambazo zimetokana na vifo vya Madiwani husika.

Kata zitakazohusika katika Uchaguzi huo na halmashauri zake ni pamoja na vijibweni – Temeke, Kiwangwa-Bagamoyo, Changombe-Dodoma, msabweni- Tanga na Kiwira-Rungwe.

Tume hiyo imesema kuwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita ndilo litakalotumika katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki na Chaguzi zote Ndogo za Madiwani ambapo pia Vituo vitakavyotumika kupiga kura ni vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2010.