MSHAMBULIAJI, Michael Victor Mgimwa ameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ili acheze soka nchini Thailand.
Chama cha Mpira wa Miguu cha Thailand (FAT) limetuma maombi hayo jana (Februari 6 mwaka huu) kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili kupata hati hiyo.
Mgimwa ambaye tayari yuko Thailand ameombewa hati hiyo ili aweze kuichezea timu ya Roiet FC ambayo iko daraja la pili nchini humo.
TFF inafanyia kazi maombi hayo na ITC itatolewa wakati wowote baada ya taratibu husika kukamilika ikiwemo kuwasiliana na Mtibwa Sugar ambayo ilikuwa klabu yake ya mwisho hapa nchini.