Na Mwandishi Wetu
LIGI Kuu ya Vodacom ambayo iko katika raundi ya 16 inaendelea kesho kwa mechi moja kati ya Yanga na Mtibwa Sugar. Mechi hiyo namba 112 itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni.
Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Ibrahim Kidiwa kutoka Tanga wakati wasaidizi wake ni Michael Mkongwa kutoka Iringa na Kudura Omary wa Tanga. Kamishna wa mechi hiyo ni Mohamed Nyange kutoka Dodoma.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP B na C, na sh. 15,000 kwa VIP A.
Wakati huo huo; timu 14 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zitakuwa kwenye viwanja saba tofauti kesho (Februari 8 mwaka huu) katika mfululizo wa ligi hiyo ambayo iko katika hatua ya makundi.
Transit Camp na Mgambo Shooting zitachuana kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga katika mechi pekee ya kundi A itakayochezeshwa na mwamuzi Said Ndege wa Dar es Salaam.
Kundi B litashuhudia mechi tatu. Tanzania Prisons itakuwa mwenyeji wa Small Kids kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, JKT Mlale itaoneshana kazi na Mbeya City kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea na Polisi Iringa itacheza na Majimaji kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.
Mechi za kundi C zitakuwa kati ya Polisi Morogoro na Morani FC itakayochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, AFC na Rhino zitacheza kwenye Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha na Polisi Tabora itakuwa mwenyeji wa 94 KJ kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.