BAADA ya miaka mingi ya mivutano na uhasama baina ya kundi la Hamas na chama cha Fatah ndani ya Palestina, hatimae makundi hayo yamefikia maridhiano ya kuwa na serikali ya mpito ya Umoja wa Kitaifa.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo huko Doha, nchini Qatar, kati ya kiongozi wa chama cha Fatah, Rais Mahmoud Abbas, na kiongozi wa Hamas, anayeishi uhamishoni, Khaled Meshaal.
Makubaliano yaliyotiwa saini hii leo yanaondoa kikwazo kimojawapo kikubwa kuelekea utekelezwaji wa makubaliano ya Umoja wa kitaifa yaliyotiwa sainia mnamo mwezi Mei yaliyolega kumaliza miaka kadhaa ya mgawanyiko miongoni mwa wapalestina.
Makubaliano hayo ya ushirikiano kati ya Hamas na Fatah yanahusisha kuundwa serikali ya mpito itakayoandaa chaguzi za bunge na rais mnamo mwezi Mei mwaka huu. Serikali hiyo itakayoongozwa na rais Mahmoud Abbas itazijumuisha pande zote mbili, ingawa bado sio wazi ikiwa itafanikiwa kuandaa uchaguzi katika wakati muwafaka.
Aidha orodha ya baraza la mawaziri wa serikali hiyp itatangazwa tarehe 18 mwezi huu. Hata hivyo, hatua ya leo imepongezwa na wasomi wengi wakipalestina, ingawa kuna mengi yanayotiliwa shaka.
Akizungumza baada ya kutia saini maafikiano hayo huko Doha kiongozi wa kundi la Hamas Khaled Meshaal amesema kwamba pande zote mbili zimejitolea katika kuufungua ukurasa mpya kwa kufikia maridhiano juu ya masuala yote. Rais Mahmoud Abbas amekariri kwamba Fatah haijasaini makubaliano hayo kwa ajili tu ya kujionesha, bali wamechukua uamuzi huo kwa lengo la kutekeleza makubaliano ya amani.
Hata hivyo, baadhi ya vyombo vya habari katika nchi za kirabu vinaripoti kwamba wako miongoni mwa wanachama wa kundi la Hamas, ambalo linalotawala ukanda wa Gaza, ambao hawajaridhika na maridhiano haya, hasa kwa rais Mahmoud Abbas kupewa wadhifa wa Waziri mkuu atakayeiongoza serikali hiyo ya mpito. Hatua hiyo huenda ikaleta mgawanyiko ndani ya kundi la Hamas.
Makubaliano ya leo yamefikiwa wakati hatima ya mazungumzo ya kusaka amani kati ya Israel na Palestina haijafahamika. Israel inasema haiwezi kukaa chini na serikali ambayo italijumuisha kundi la Hamas, ikilitaja kuwa ni kundi la magaidi.
Kundi hilo, kwa upande wake, limekataa katakata hadi sasa kuitikia matakwa ya jumuiya ya Kimataifa ya kuitambua haki ya kuweko taifa la Israel na kuacha matumizi ya nguvu dhidi ya taifa hilo la Kiyahudi. Rais Obama ameshasema leo kwamba anataka kuiona serikali ya Palestina ambayo itatambua haki ya kuweko kwa dola ya Israel.
Hivi punde Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ametoa kauli yake akiikosoa hatua ya Rais Abbas akisema amechagua njia ya kuyatupa mkono mazungumzo ya amani na Waisraeli.
-DW