Na John Mnyika
NAWASHUKURU wote walioitikia NDIYO (kwa kujua au kutokujua) kuunga mkono marekebisho mengine ambayo niliyawasilisha katika sheria husika ya kuongeza ukubwa wa adhabu kutoka na makosa ya ujumla ya kukiuka Sheria ya Udhibiti wa Fedha haramu.
Niliwasilisha marekebisho kwenye sheria ili pamoja na kifungo watakaobainika kufanya makosa hayo watozwe ambayo ni sawa na kiwango cha fedha kilichohusika au kiwango cha thamani halisi ya soko ya mali iliyohusika. ( or be ordered to pay the amount equivalent to total amount of money involved or market value of the property, which is greater).
Nilisisitiza kwamba kifungu hicho ni muhimu kikaingizwa kwa kuwa fedha haramu zinaathari kubwa sana katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi na kushindwa kuzikabili kunarudisha nyuma vita dhidi ya ufisadi, madawa ya kulevya, ugaidi, uharamia na kwamba kushindwa kukabiliana na hali hiyo kunachangia katika mfumuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania.
Katika maelezo yake ya kukataa kifungu hicho cha nyongeza ya adhabu Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema kwamba kifungo cha miaka mitatu kinatosha kwa makosa hayo na kwamba scheme ya adhabu niliyoipendekeza ni tofauti na inakinzana na penal code.
Katika majibu yangu kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali nilimweleza kwamba nyongeza ya adhabu dhidi ya makosa ya fedha haramu hakiwezi kukinzana na penal code, na kama hoja ya kukinzana na penal code ingekuwa ni ya msingi basi hoja hiyo hiyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali angeitumia kuzuia kuwekwa kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kifungu kinachoruhusu wananchi watakaokutwa na makosa ya kutoa elimu juu ya mabadiliko ya katiba au kukusanya maoni juu ya katiba mpya kufungwa kwa miaka saba. Hivyo, haiwezekani anayefanya kosa la fedha haramu akafungwa miaka mitatu lakini anayetoa elimu au kukusanya maoni akafungwa kwa miaka saba.
Pia, nilimtaka Mwanasheria mkuu azingatie kwamba marekebisho niliyoyatoa siyo ya scheme tofauti kwa kuwa sheria ya fedha haramu kwa kadiri ilivyo sasa kifungu cha 13 kimeweka adhabu yenye mwelekeo wa faini kulingana na thamani ya mali, hivyo marekebisho niliyowasilisha yalilenga kupanua wigo wa adhabu hizo kwa makosa ya ujumla pamoja na kuongeza ukubwa wa adhabu.
Baada ya majibu hayo, Mwenyekiti wa Bunge Mheshimiwa Mabumba akahoji ‘kifungu hicho kinapatishwa pamoja na marekebisho yake?” Na wabunge wakaitikia NDIO. Baada ya kifungu kupitishwa na bunge kumaliza kukaa kama kamati, Bunge lilirejea na kupokea taarifa ya kazi kukamilika.
Hivyo, muswada ukapitishwa baada ya kusomwa kwa mara ya pili, ya tatu pamoja na marekebisho yaliyofanyika. Mwenyekiti wa bunge akatangaza kwamba muswada umeshapitishwa na bunge katika hatua zake zake zote. Baada ya bunge kukamilisha hatua zake ndipo Mbunge wa Simanjiro Mh. Ole Sendeka akaomba muongozo ambapo ulimfanya Mwenyekiti atangaze kufuta maneno aliyoyasema wakati bunge lilipokaa kama kamati “pamoja na marekebisho yake”.
Ni imani yangu kwamba kufutwa kwa maneno hayo katika hatua ya baadaye hakuwezi kuathiri maamuzi ya bunge ambayo yalishafanywa na bunge kwa kura wakati wa kamati na baada ya kamati. Bunge litaingia katika historia ya aibu iwapo litafuta muswada wa sheria ambayo tayari ulishapitishwa na bunge kwa kauli tu ya mwenyekiti.
Pia, sheria hiyo ikibadilishwa na kutungwa tofauti na ilivyopitishwa pamoja na marekebisho niliyowasilisha ya kuongeza ukubwa wa adhabu itakuwa ni ushahidi tosha kwamba wabunge wa CCM hupiga kura ya NDIO bila hata kujua wanapigia kura suala gani.
Kwangu mimi makosa hapa hayakuwa ya mwenyekiti bali wabunge ambao watabadili msimamo wao wa mwanzo wa kupiga kura ya NDIO baada ya mwenyekiti kuhoji ‘pamoja na marekebisho yake’ kwa kigezo tu cha kuwa mwenyekiti alikosea maneno hayo. Kama wangekuwa na dhamira ya kweli ya kukataa kifungu husika wangesikiliza hayo maneno ‘pamoja na marekebisho yake’ na kupiga kura ya SIYO badala ya NDIYO kama walikuwa wanayapinga. Tukio hili lisipochukuliwa kwa umakini linaweza kuiweka hadhi ya bunge mashakani kuhusu wajibu wake wa kikatiba wa kutunga sheria.
Hata hivyo, izingatiwe kuwa uwepo wa sheria pekee hauwezi kutatua changamoto tulizonazo bila ya kusimamia kwa sheria husika. Changamoto kubwa tuliyonayo kama taifa ni kutetereka kwa misingi ya uwajibikaji na kupuuzwa kwa utawala wa sheria. Hivyo, tuendelee kuunganisha nguvu ya umma kuhakikisha kwamba nchi inaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria zilizo bora.