WATU wapatao 37 wameuawa nchini Sudan Kusini baada ya kushambuliwa kwa risasi kwenye mkutano wa amani unaolenga kumaliza ghasia katika eneo hilo, wamesema maofisa nchini humo.
Maofisa kutoka majimbo matatu walikutana katika mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa katika mji wa Mayendit, kwenye jimbo la Unity, katika jitihada za kupunguza uhasama wa kikabila.
Taarifa zaidi kutoka Sudan Kusini, zinasema kuwa kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), magari manne yaliwasili eneo la mkutano yakiwa yamejaa askari polisi ambao mara moja walianza kufyatua risasi.
Miongoni mwa waliokufa ni raia. Wanaharakati wa haki za binaadam wameshutumu ukosefu wa nidhamu miongoni mwa majeshi ya usalama.
Mazungumzo hayo yaliitishwa kufuatia mfululizo wa mapigano, yakiwemo mapigano ambayo watu 74 waliuawa mapema wiki hii. Mamia ya watu wamekimbia makazi yao kutokana na ghasia hizo.
-BBC