Wizara ya Ujenzi yakanusha malipo hewa mkandarasi

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuli

KATIKA gazeti la Raia Mwema la tarehe 1 Februari 2012 iliandikwa taarifa na Mwandishi aliyejitambulisha kwa jina la Mwandishi wetu akidai kuwepo kwa malipo hewa kwa Mkandarasi M/s CHICO- CRSG JV anayejenga barabara ya Kagoma – Lusahunga kwa kiwango cha lami.

Taarifa hizi siyo sahihi, hivyo tunapenda kutoa taarifa sahihi kwa umma kuhusiana na suala hili kama ifuatavyo; Barabara ya Kagoma – Lusahunga yenye urefu wa kilomita 154 inajengwa kwa kiwango cha lami.
Mkataba wa ujenzi wa Barabara hii ulisainiwa kati ya Wakala wa Barabara (TANROADS) na Mkandarasi M/S CHICO-CRSG JV mnamo tarehe 18 Juni 2009. Gharama ya ujenzi wa barabara hii ni Shilingi bilioni 191.454 ambayo inajumuisha kodi zote. Kazi za ujenzi zimepangwa kufanyika kwa muda wa miezi 36 na fedha zote zinatolewa na Serikali ya Tanzania.

Mradi huu unasimamiwa na Mhandisi Mshauri M/s Intercontinental Consultants & Technocrats Pvt (ICT) wa India kwa gharama ya Dola za marekani milioni 1.071 na Shilingi za Kitanzania bilioni 1.698 ambayo ni sawa na jumla ya Shilingi bilioni 3.396. Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 60 ambapo jumla ya kilomita 88 zimeshawekwa lami kati ya kilomita 154.

Hadi mwezi Novemba 2011 wakati tunafanya maandalizi ya malipo ya mwisho, Mkandarasi alikuwa amewasilisha hati za madai (Interim Payment Certificates) nane (8) za jumla ya Shilingi bilioni 27.224
Baada ya kupata fedha kiasi cha shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kulipa madeni ya Makandarasi, Mkandarasi M/s CHICO-CRSG JV alilipwa shilingi 5,783,883,829.45 na USD 6,484,615.43 (sawa na shilingi 10,282,460,141.24 kwa exchange rate ya 1 USD = 1,585.6700).

Jumla ya fedha alizolipwa ni shilingi 16,066,343,970.69 ambayo ni sawa na asilimia 59% ya deni alilokuwa anadai wakati huo. Hivyo, hakuna malipo yoyote hewa yaliyofanyika kwa mkandarasi CHICO-CRSG JV.
Malipo ya madeni ya mkandarasi yanafanyika kwa kutumia hati za madai (Interim Payment Certificates) iliyoidhinishwa na Mhandisi Mshauri anayesimamia mradi husika. Aidha, hati hizo huwasilishwa TANROADS ambao nao huzipitia. Baada ya hapo hati hizo huwasilishwa Wizarani kwa ajili ya kuombea fedha za malipo kutoka Hazina. Malipo haya hayana uhusiano na maandalizi yeyote ya kampeni za uchaguzi kama ambavyo taarifa ya gazeti imetaka wasomaji wake waamini.

Kuhusiana na mabadiliko ya uongozi ndani ya Wizara, Wakala wa Barabara na taasisi nyingine zilizopo chini ya Wizara, ni muhimu kufahamu kwamba mabadiliko yanafanyika kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi. Aidha, mabadiliko hufanyika kwa kuzingatia sheria taratibu na kanuni za Serikali. Kwa kuwa mabadiliko yoyote huwagusa watu kwa njia mbalimbali, malalamiko yanaweza kuwepo miongoni mwa baadhi yao. Hata hivyo, Wizara na taasisi zake zitaendelea kufanya mabadiliko kwa kadri mahitaji yatakavyojitokeza katika kuimarisha utendaji na ufanisi wa kazi.

Mabadiliko haya yameanza kuonyesha ufanisi katika utendaji wa majukumu ya kazi mbalimbali ndani ya Wizara na taasisi zake.
Mwisho, tunapenda kutoa rai kwamba ili vyombo vya habari viweze kutoa taarifa sahihi na ambazo hazipotoshi umma, ni vema viwasiliane na wasemaji wa Wizara na taasisi zake ili kupata taarifa sahihi na za ukweli.

Imetolewa na Balozi Herbert E. Mrango, KATIBU MKUU – WIZARA YA UJENZI