Dk Shein kuiongezea uwezo Idara Maalumu za Vikosi vya SMZ

Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amesema ipo haja ya Serikali yake kuiongezea uwezo Idara Maalumu za Vikosi vya SMZ kiutendaji kwa kuwapatia mafunzo wapiganaji wake ndani na nje ya nchi ili kuvifanya vikosi hivyo kuwa na wataalamu pamoja na kwenda na wakati.

Dk. Shein aliyasema hayo leo alipokutana na uongozi wa Idara Maalumu za Vikosi vya SMZ chini ya Waziri wake, Dk. Mwinyihaji Makame, Ikulu mjini Zanzibar. Mkutano huo ni muendelezo wa kukutana na Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuangalia Mpango Kazi wa utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/12 kwa kipindi cha robo ya kwanza na ya pili ya mwaka.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa hatua ya Idara hiyo Maalum za Vikosi vya SMZ itaweza kuviimarisha zaidi vikosi vyake kwa kuwa na wataalamu wa kada mbali mbali sanjari na kuweza kuwavutia vijana wasomi kuweza kujiunga na vikosi hivyo.

Dk. Shein alieleza kuvutiwa kwake na hatua hiyo ya kuviongezea uwezo wa kiutendaji vikosi hivyo ambayo kutavifanya vikosi hivyo kwenda na wakati uliopo wa sayansi na teknolojia. Dk. Shein aliipongeza Idara hiyo kwa jitihada kubwa waliyoichukua katika kupambana na magendo ya karafuu chini ya kikosi kazi ‘Task force’, hatua ambayo imesaidia kuokolewa kwa kiasi kikubwa kwa zao hilo la karafuu na kuweza kuuzwa kwa serikali hali ambayo imeweza kuongeza nguvu katika uchumi wa nchi.

Aidha alitoa pongezi zake kwa kazi inazifanya vikosi hivyo ikiwa ni pamoja na kuiamrisha amani na utulivu hali ambayo inatokana na kuwa na viongozi na makamanda hodari.

Kwa upande wao uongozi wa Ofisi hiyo ulieleza kfarajika kwao na juhudi anazozichukua Dk. Shein katika uongozi wake na kutoa salam za pongezi kutoka kwa wapiganaji wote wa vikosi vya SMZ kutokana na hatua za Dk. Shein za kutimiza ahadi yake ya kuwaongezea mishahara wafanyazi wa sekta ya umma ambao nao wamefaidika na kufurahishwa na hatua hiyo.

Uongozi huo ulieleza kufurahishwa na hatua za Dk. Shein za kufanya ziara za kuvitembelea vikosi vyote katika maeneo yao na kuona mafanikio na changamoto zilizopo mara baada ya kuingia madarakani, hatua ambayo imeonesha ni kwa jinsi gani amekuwa akivijali vikosi vya SMZ kwa kutambua umuhimu wake katika kuimarisha amani na utulivu pamoja na sekta za maendeleo hapa nchini.

Akisoma utangulizi juu ya taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi hiyo, Waziri Mwinyihaji alisema kuwa Idara hizo zimeendelea kusimamia ulinzi na usalama wa visiwa vya Zanzibar ambapo mkazo zaidi umewekwa kwa kuwapatia mafunzo makamanda na maaskari yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Aidha, uongozi huo ulipongeza juhudi za Dk. Shein za kuendelea kuziunga mkono timu za michezo za Idara hizo ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika mashindano kadhaa. Pamoja na hayo, uongozi huo ulieleza kuwa licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto katika vikosi hivyo lakini juhudi zimekuwa zikichukuliwa na serikali katika kuzitatua awamu kwa awamu.

Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na Uongozi wa Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora chini ya Waziri wake Mhe. Haji Omar Kheir ambaye alisoma utangulizi wa taarifa juu ya utekelezaji wa malengo ya Ofisi hiyo ya Rais na kueleza vipaumbele ilivyoviweka.

Aidha, Mhe. Kheir alieleza kuwa Ofisi hiyo ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa Watumishi wa Umma ili kuwahudumia wananchi kwa kiwango cha juu, kuleta ufanisi na kuimarisha Utawala Bora nchini.

Pia, alieleza kuwa Ofisi hiyo ina jukumu la kusimamia, kudhibiti, kuratibu na kutathmini utekekelezaji na uongozaji wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kuzingatia misingi ya mipango ya kitaifa kama vile Dira ya 2020, MKUZA II, Ilani ya Uchaguzi ya CCM na 2010-2015 pamoja na mikataba na makubaliano ya kikanda na kimataifa ambayo imeridhiwa nchini.

Katika kuwajengea uwezo wananchi juu ya dhana nzima ya uelewa wa Utawala Bora, Waziri Kheir alisema kuwa elimu ya uraia kwa umma kupitia vipindi vya redio, semina na makongamano imetolewa mjini na vijini. Waziri huyo alieleza kuwa muongozo wa uhakiki wa wafanyakazi na mishahara umetayarishwa, muongozo huo unasaidia kuwatambua wafantyakazi halali wa Serikali na kudhibiti upotevu wa fedha za Serikali kulipia mishahara hewa.

Pia, alieleza kuwa Serikali inajukumu kubwa la kuwawekea mazingira mazuri watumishi wake na kuhakikisha wanapata maendeleo katika Nyanja tofauti ikiwemo maslahi yanayolingana na kukua kwa uchumi. Alieleza kuwa katika kufanikisha azma hiyo, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetayarisha na kutekeleza miundo mipya ya mishahara ya watumishi wa umma ambayo imezingatia uzoefu na taaluma za watumishi.

Kwa upande wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Waziri huyo alieleza kuwa Ofisi imeendelea na majukumu yake ya ukaguzi wa mahesabu ya mwaka 2009/2010/2011 katika taasisi mbali mbali za serikali kwa kufuata muongozo wa ukaguzi.

Naye Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee ambaye amekuwa akishiriki kikamilifu katika vikao hivyo tokea kuanza kwake alieleza haja ya kuendeleza mashirikiano ya pamoja katika kuimarisha kazi za Ofisi hiyo.

Akizungumza na uongozi huo Dk. Shein alitoa pongezi kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kuwasilisha Bangokitita ‘Matrix’ la Wizara hiyo kwa robo mbili sanjari na kusimamia vyema majukumu ya kazi zao za kila siku na mafanikio makubwa yaliopatikana nchini ikiwa ni pamoja na kufanikisha taratibu za maslahi kwa wafanyakazi wa sekta za umma.