Dk Shein kutembelea Uturuki

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuondoka nchini Aprili 28 kuelekea Jamhuri ya Uturuki kwa ziara ya mwaliko wa rais wa nchi hiyo, Abdullah Gul.

Katika ziara hiyo, Dk. Shein atafuatana na Mkewe Mama Mwanamwema Shein, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdalla Shaaban na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Jihadi Hassan.

Wengine ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Mahadhi, Mkurugenzi Mwendeshaji ZIPA, Salum Khamis Nassor pamoja na Maafisa wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika ziara yake hiyo, Dk. Shein ataweka shada la maua katika kaburi la muasisi wa Jamhuri ya Uturuki marehemu Kemal Atyaturk kabla ya mapokezi rasmi katika makaazi ya Rais ambapo pia, atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Abdullah Gul na viongozi wengine.

Akiwa nchini Uturuki Dk. Shein atatembelea Chuo cha Utafiti wa Tiba kiliopo Ankara na baadae atazuru Bunge la Uturuki na kukutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Uturuki Mehmet Ali Sahin. Baada ya mazungumzo hayo Dk. Shein atakuwa na mahojiano na radio na televisheni ya Taifa ya Uturuki TRT.

Wakati wa usiku Dk. Shein atahudhuria dhifa maalum iliyoandaliwa kwa heshima yake na Rais wa Jamhuri ya Uturuki Mhe. Abdullah Gul.

Aidha, Dk. Shein katika ziara yake hiyo anatarajiwa kutembelea Jimbo la Antalya ambako pamoja na shughuli nyengine atatembelea kituo cha Utafiti wa Kilimo ‘West Mediterranean Agricultural Research Centre’ na kuona maeneo ya asili ambayo ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii nchini Uturuki.

Naye Mama Mwanamwema Shein amepangiwa kutembelea Taasisi za kazi za mikono zilizopo Ankara, Jumba la makumbusho pamoja na kushiriki katika baadhi ya shukughuli