Rais Kikwete akutana na Baraza la NGO’s taifa

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea mapendekezo ya Baraza la Taifa la NGOs Ikulu jijini Dar es Salaam leo Januari 3, 2012 kuzungumzia mchakato wa Katiba. PICHA NA IKULU.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na ujumbe wa Asasi Zisizokuwa za Kiserikali (AZISE) wamekutana Februari 3, 2012, Ikulu, Dar es Salaam, kuzungumzia mapendekezo ya Asasi hizo kuhusu jinsi ya kuboresha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Nambari 8 ya Mwaka 2011.
Ujumbe huo wa watu 17 na ulioongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la AZISE, Humphrey Polepole umefanya mazungumzo ya kiasi cha saa tatu na Rais Kikwete na kutoa mapendekezo yake juu ya kuboresha Sheria hiyo na mchakato nzima wa kutungwa kwa Katiba Mpya.
Mbali na Polepole, ujumbe huo ulishirikisha pia wajumbe wengine saba wa Baraza hilo, na wajumbe kutoka taasisi za Tanzania Youth Coalition (TYC), mjumbe kutoka The Leadership Forum/Jukwaa la Katiba, SHIVYAWATA, FEM ACT, mjumbe kutoka Legal and Human Rights Centre/Jukwaa la Katiba, SAHRINGON, na Youth of United Nations (YUNA).

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikutana na viongozi wa Baraza la Taifa la NGOs Ikulu jijini Dar es Salaam leo Januari 3, 2012 kuzungumzia mchakato wa Katiba. PICHA NA IKULU.


Mazungumzo kati ya Rais Kikwete na ujumbe huo yamefanyika katika mazingira ya maelewano na miongoni mwa mambo mengine pande hizo mbili zimekubaliana mambo matatu; moja likiwa kwamba ujumbe wa wataalam wa ASIZE kukutana mara moja na ujumbe wa watalaam wa Serikali kuona namna gani ya kushirikisha mawazo ya Asazi hizo katika mchakato unaoendelea wa Marekebisho ya Sheria na ule mpana zaidi wa Katiba yenyewe.
Lingine ni Katiba inayotafutwa ni Katiba ya Watanzania wote na ya nchi ya Tanzania, na wala siyo ya chama kimoja cha siasa, ama ya kabila moja ama ya kikundi kimoja cha dini. Hivyo, Katiba hiyo itafutwe kwa kujali na kutilia maanani kulinda Umoja na mustakabali wa Taifa. Huku la tatu ikiwa ni kuhakikisha kila mwananchi ana uhuru kamili kushiriki katika Mchakato wa Kutunga Katiba Mpya lakini uhuru huo utumike kusaidia kufanikisha mchakato na wala siyo kuvuruga nchi.
Ujumbe huo pia umempongeza Mheshimiwa Rais Kikwete kwa ujasiri wake wa kuanzisha mchakato wa Kutafuta Katiba Mpya kwa namna ambayo haijapata kufanyika tokea kupatikana kwa Uhuru miaka 50 iliyopita na kufanikiwa kwa Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964.
Rais Kikwete mwenyewe amewashukuru wajumbe hao kwa kukubali kukutana naye kujadili suala muhimu kwa maslahi ya nchi na kusema kuwa utashi wake ni kuona Tanzania inapata Katiba nzuri na inayotelekezeka na kwa wakati uliokubaliwa.
Hili ni kundi la nne kukutana na Mheshimiwa Rais Kikwete kuhusiana na mchakato huo. Kabla ya hapo, Rais Kikwete amekutana na kufanya majadiliano na uongozi wa vyama vya siasa vya CHADEMA, CUF na NCCR.