PAMBANO la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Oljoro JKT lililochezwa Februari Mosi mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 40,191,000. Jumla ya watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 105 kwa kiingilio cha sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000 kwa VIP A walikuwa 11,860.
Taarifa ya TFF leo kwa vyombo vya habari imesema kiasi hicho cha fedha kimepatikana baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kila timu ilipata sh. 7,023,171, uwanja sh. 2,341,057, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 936,423, TFF sh. 2,341,057, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,170,528 na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 234,106.
Aidha taarifa hiyo imeendelea kubainisha kuwa mechi namba 104 kati ya African Lyon na Polisi Dodoma iliyochezwa Februari Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam imeingiza sh. 45,000 kutokana na watazamaji 15 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo.
Baada ya kuondoa asilimia 18 ya VAT ambayo ni sh. 6,864.41 kila timu ilipata sh. 2,591, Uwanja sh. 514, TFF sh. 514, DRFA sh. 205, FDF sh. 257 na BMT sh. 51.
WAKATI huo huo TFF wamesema mzunguko wa pili (second leg) wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayochezwa katika makundi matatu tofauti unaanza kesho (Februari 4 mwaka huu) kwa mechi sita.
Katika kundi A, Morani FC itakuwa mwenyeji wa Burkina Faso ya Morogoro katika mchezo utakaochezwa Kiteto mkoani Manyara. Kwa upande wa kundi B timu zote sita zitakuwa uwanjani.
Small Kids ya Rukwa itacheza na Polisi ya Iringa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Mbeya City na Tanzania Prisons zitaumana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya na Majimaji na Mlale JKT watapepetana katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Kundi C litaanza kwa mechi mbili ambapo AFC ya Arusha watakuwa wageni wa Manyoni mkoani Singida na Rhino na Polisi Tabora zitakwaruzana kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Mechi nyingine ya kundi hilo itakuwa kati ya 94 KJ na Polisi Morogoro ambayo itachezwa keshokutwa (Februari 5 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.