Na Joachim Mushi
SUALA la mgogoro wa aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoani Mara (FAM), Michael Wambura ambaye baadaye alienguliwa na Kamati ya Uchaguzi TFF limeendelea kulikanganya shirikisho hilo, na sasa imeamua kuomba msaada wa kisheria.
Jana Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Oseah ameamua kuiandikia barua Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji akiomba apewe ushauri wa kisheria juu ya namna ya kulishughulikia suala hilo.
Katika barua yake Katibu huyo alihoji kitendo cha Kamati ya Rufaa kufanya uamuzi wa kumrejesha Wambura katika uchaguzi ilhali maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ni ya mwisho na hayapaswi guhojiwa na chombo chochote.
Alisema japokuwa uamuzi huo wa kumrejesha Wambura katika uchaguzi ulikuwa umechelewa, baada ya kufanyika tayari kwa uchaguzi wa FAM; jambo hilo limekuwa na mkanganyo hivyo Sekretarieti ya TFF kupitia kwa katibu kuona kuna haja ya chombo hicho kulitolea mwongozo suala hilo.
“…Kamati ya Rufaa ilieleza kuwa Wambura alistahili kurejeshwa kwenye Uchaguzi wa FAM, lakini ilichelewa kumrejesha kwa kuwa uchaguzi ulikwishafanyika jambo ambalo Sekretarieti inaliona halikuwa sahihi kwa kuwa Kamati ya Uchaguzi imepewa mamlaka ya kuingilia mchakato wa uchaguzi wa vyama wanachama wake wakati wowote na kufanya maamuzi hata kama hakuna rufaa, kama ilivyofanya kwa uchaguzi wa FAM, Simba, Coastal Union, Villa Squad,” alisema Katibu huyo wa TFF.
“Ili kuondoa uwezekano wa kuendelea kuendelea kwa ukakasi baina ya vyombo vya maamuzi vya TFF, tunaiomba Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kupitia suala hili na kutoa ushauri wa kisheria jinsi ya kuendelea nalo katika ngazi nyingine,” amesema Oseah.