Njia ya kupambana na makali ya maisha ni kuchapa kazi-Pinda

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imesema ili kukabiliana na tatizo la mtikisiko wa uchumi uliotokea pamoja na mfumuko wa bei Watanzania wanatakiwa kufanyakazi kwa bidii zaidi hasa katika uzalishaji wa chakula. Imesema kupatikana kwa chakula kwa wingi kutasababisha bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei ndogo hivyo kumpa hauweni mtumiaji.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo mjini Dodoma na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa akijibu maswali ya papo hapo toka kwa wabunge. Hata hivyo Pinda amekiri kuwa Tanzania kwa sasa inapitia katika kipindi kigumu kiuchumi kutokana na sababu anuai.

Aidha amesema, Waziri Mkuu amesema ili kukabiliana na tatizo hilo Serikali imeelekeza nguvu zake kwenye kilimo kama njia ya kuongeza ajira hasa kwa vijana. Akizungumzia huduma kwa waathirika wa mafuriko jijini Dar es Salaam kwa sasa, Waziri Mkuu Pinda baada ya kuulizwa bungeni; amesema tayari Serikali imeshapima na kugawa zaidi ya viwanja 300 kwa waathirika hao.

Aliongeza kuwa Serikali inafanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha inapata viwanja kwa ajili ya kuwagawia waliokuwa wapangaji kwenye nyumba zilizoathiriwa na mafuriko hayo. Pinda alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee aliyetaka kujua utekelezaji wa agizo la rais la kugawa viwanja kwa waathirika wa mafuriko hayo.