Na Zawadi Msalla-Maelezo
RAIS Jakaya Kikwete kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, yatakayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Mahakama ya Rufaa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman alisema maadhimisho hayo yatalenga katika kujadili masuala mbalimbali ya kisheria ili kutoa elimu kwa wananchi kwa ujumla.
Jaji Mkuu aliongeza kuwa wananchi wengi wanapoteza haki zao za msingi kwa kutokujua sheria, hivyo kuna umuhimu kwa wao kupewa fursa ya kujua aina za makosa na adhabu zinazoweza kutolewa katika makosa hayo.
“Tangu kuanzishwa kwa sherehe hizi, zimelenga zaidi katika kuhakikisha wananchi wanajua mambo mbalimbali ya kisheria yanayowahusu, kwani wengi huwa wanapoteza haki zao za msingi kwa kutokujua sheria, lazima tuelewe kwamba kutokujua sheria haina msamaha katika kosa,” alisema Jaji Mkuu.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni adhabu Mbadala katika kesi za Jinai: Faida zake katika jamii. Shereha hizo pia zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi anuai wakiwemo wa vyama na Serikali, na Rais wa Chama cha Mawakili nchini.